40
Kuweka wakfu maskani ya Mungu
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: “Simika maskani ya Mungu, lile Hema la Kukutania, katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza. Weka Sanduku la Ushuhuda ndani yake na ulifunike kwa pazia. Ingiza meza na kupanga vitu vyake juu yake. Kisha ingiza kinara cha taa na uweke taa zake juu yake. Weka madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba mbele ya Sanduku la Ushuhuda kisha uweke pazia kwenye lango la maskani ya Mungu.
“Weka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa mbele ya lango la maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania; weka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, na uweke maji ndani yake. Tengeneza ua kuzunguka maskani ya Mungu, na uweke pazia penye ingilio la ua.
“Chukua mafuta ya upako, upake maskani ya Mungu pamoja na kila kitu kilicho ndani yake; iweke wakfu pamoja na vitu vyote vilivyomo, nayo itakuwa takatifu. 10 Kisha yapake mafuta hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka pamoja na vifaa vyake vyote; weka wakfu madhabahu nayo yatakuwa takatifu sana. 11 Paka sinia mafuta pamoja na kishikilio chake na uviweke wakfu.
12 “Mlete Haruni na wanawe kwenye ingilio la Hema la Kukutania na uwaoshe kwa maji. 13 Kisha mvike Haruni yale mavazi matakatifu, umpake mafuta na kumweka wakfu ili apate kunitumikia kama kuhani. 14 Walete wanawe na uwavike makoti. 15 Kisha wapake mafuta kama ulivyomtia baba yao, ili nao pia wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Kupakwa mafuta kwao kutakuwa kwa ajili ya ukuhani utakaoendelea kwa vizazi vyote vijavyo.” 16 Musa akafanya kila kitu sawa kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
17 Kwa hiyo maskani ya Mungu ilisimikwa katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, katika mwaka wa pili. 18 Musa alipoweka wakfu maskani ya Mungu, aliweka vitako mahali pake, akasimamisha mihimili, akatia mataruma na kusimamisha nguzo. 19 Kisha akalitandaza hema juu ya maskani ya Mungu na kuifunika hema, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
20 Akachukua ule Ushuhuda na kuuweka ndani ya Sanduku la Agano, akaweka ile mipiko ya kubebea hilo Sanduku na kuweka kiti cha rehema juu yake. 21 Kisha Musa akalileta Sanduku ndani ya maskani ya Mungu, akatundika pazia ili kulifunika Sanduku la Ushuhuda, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
22 Musa akaweka meza ndani ya Hema la Kukutania, upande wa kaskazini mwa maskani ya Mungu nje ya pazia 23 na kupanga mikate juu yake mbele za Mwenyezi Mungu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
24 Akaweka kinara cha taa ndani ya Hema la Kukutania mkabala na meza upande wa kusini mwa maskani ya Mungu 25 na kuziweka taa mbele za Mwenyezi Mungu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
26 Musa akaweka madhabahu ya dhahabu ndani ya Hema la Kukutania mbele ya pazia, 27 na akafukiza uvumba wenye harufu nzuri, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza. 28 Kisha akaweka pazia kwenye ingilio la maskani ya Mungu.
29 Musa akaweka madhabahu ya sadaka za kuteketezwa karibu na ingilio la maskani ya Mungu, yaani Hema la Kukutania, na kutoa juu yake sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza.
30 Akaweka sinia kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, akaweka maji ndani yake kwa ajili ya kunawia. 31 Naye Musa, Haruni na wanawe wakayatumia kwa kunawia mikono na miguu yao. 32 Wakanawa kila walipoingia katika Hema la Kukutania au walipoikaribia madhabahu, kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa.
33 Kisha Musa akatengeneza ua kuizunguka maskani ya Mungu na madhabahu, na pia akaweka pazia kwenye ingilio la huo ua. Hivyo Musa akaikamilisha kazi.
Utukufu wa Mwenyezi Mungu
(Hesabu 9:15-23)
34 Ndipo wingu likafunika Hema la Kukutania, na utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaijaza maskani ya Mungu. 35 Musa hakuweza kuingia ndani ya Hema la Kukutania kwa sababu wingu lilikuwa limetua juu ya Hema, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukaijaza maskani ya Mungu.
36 Katika safari yote ya Waisraeli, kila wakati wingu lilipoinuka kutoka juu ya maskani ya Mungu, wangeondoka; 37 lakini kama wingu halikuinuka, hawakuondoka, hadi siku lilipoinuka. 38 Kwa hiyo wingu la Mwenyezi Mungu lilikuwa juu ya maskani ya Mungu mchana, na moto ulikuwa katika hilo wingu wakati wa usiku, machoni pa nyumba yote ya Israeli siku zote za safari zao.