2
Wito wa Ezekieli
Akaniambia, “Mwanadamu, simama kwa miguu yako nami nitasema nawe.” Alipokuwa akiongea nami, Roho wa Mungu akanijia na kunisimamisha wima, nikamsikia akisema nami.
Akaniambia: “Mwanadamu, ninakutuma kwa Waisraeli, taifa ambalo limeniasi mimi; wao na baba zao wameniasi hadi leo. Watu ninaokutuma kwao ni wakaidi na wabishi. Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mungu Mwenyezi.’ Kama watasikiliza au hawatasikiliza, kwa kuwa wao ni nyumba ya uasi, watajua nabii amekuwa miongoni mwao. Nawe mwanadamu, usiwaogope wao wala maneno yao. Usiogope, ijapo michongoma na miiba vinakuzunguka na unaishi katikati ya nge. Usiogope yale wasemayo wala usitishwe nao, ijapo wao ni nyumba ya uasi. Lazima uwaambie maneno yangu, ikiwa watasikiliza au hawatasikiliza, kwa kuwa wao ni waasi. Lakini wewe mwanadamu, sikiliza ninalokuambia. Usiasi kama hiyo nyumba ya uasi. Fungua kinywa chako na ule nikupacho.”
Ndipo nikatazama, nami nikaona mkono ulionyooshwa kunielekea. Nao ulikuwa na kitabu, 10 ambacho alikikunjua mbele yangu. Pande zote mbili kilikuwa kimeandikwa maneno ya maombolezo, na vilio na ole.