Ezekieli
1
Viumbe hai na utukufu wa Mwenyezi Mungu
Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa miongoni mwa waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu.
Katika siku ya tano ya mwezi, mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehoyakini, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa juu yake.
Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini: wingu kubwa sana likiwa na miali ya radi, likizungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama chuma inavyong’aa ndani ya moto. Ndani ya ule moto kulikuwa na mfano wa viumbe wanne wenye uhai. Kuonekana kwao walikuwa na umbo la mwanadamu, lakini kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyooka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja; hawakugeuka walipotembea.
10 Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa hao wanne alikuwa na uso wa mwanadamu, na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, na kwa upande wa kushoto alikuwa na uso wa ng’ombe; pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai. 11 Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliokunjuliwa kuelekea juu; kila bawa liligusa bawa la mwenzake kila upande; kila mmoja wao alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake. 12 Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja. Popote roho alipoenda, walienda pasipo kugeuka. 13 Kuonekana kwa wale viumbe hai kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya wale viumbe; ulikuwa na mwangaza mkali na katika ule moto kulitoka miali ya radi. 14 Wale viumbe walipiga mbio kwenda na kurudi, kama miali ya radi.
15 Nilipokuwa nikitazama wale viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe na nyuso zake nne. 16 Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yalimetameta kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilionekana kuwa na gurudumu lingine ndani yake. 17 Magurudumu yalipoenda, yalielekea upande mmoja wa pande nne walikoelekea wale viumbe; wale viumbe walipoenda, magurudumu hayakugeuka. 18 Kingo za magurudumu zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote.
19 Wale viumbe hai walipoenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea; wakati hao viumbe hai walipoinuka kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka. 20 Popote roho alipoenda, wale viumbe nao walienda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa sababu roho ya wale viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu. 21 Viumbe wale waliposogea, nayo magurudumu yalisogea; viumbe waliposimama, nayo pia yalisimama; viumbe walipoinuka juu ya nchi, magurudumu yaliinuka pamoja nao, kwa kuwa roho ya hao viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.
22 Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na la kutisha. 23 Chini ya hiyo nafasi, mabawa yao yalitanda moja kuelekea lingine, na kila mmoja alikuwa na mabawa mawili yaliyofunika mwili wake. 24 Viumbe wale waliposogea, nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi*Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania., kama kishindo cha jeshi. Waliposimama, walishusha mabawa yao.
25 Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa. 26 Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha utawala cha yakuti samawi. Na juu ya kile kiti cha utawala kulikuwa na umbo, mfano wa mwanadamu. 27 Nikaona kwamba kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea juu, alionekana kama chuma inavyong’aa ikiwa ndani ya moto, na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto; mwanga wenye kung’aa sana ulimzunguka. 28 Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mng’ao uliomzunguka.
Hivi ndivyo mfano wa utukufu wa Mwenyezi Mungu ulionekana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

*1:24 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.