5
Kumbuka, Ee Mwenyezi Mungu, yaliyotupata,
tazama, nawe uione aibu yetu.
Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni,
na nyumba zetu kwa wageni.
Tumekuwa yatima wasio na baba,
mama zetu wamekuwa kama wajane.
Ni lazima tununue maji tunayokunywa,
kuni zetu zapatikana tu kwa kununua.
Wanaotufuatilia wapo kwenye visigino vyetu,
tumechoka na hakuna pumziko.
Tumejitolea kwa Misri na Ashuru
tupate chakula cha kutosha.
Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena,
na sisi tunachukua adhabu yao.
Watumwa wanatutawala
na hakuna wa kutuokoa mikononi yao.
Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu
kwa sababu ya upanga jangwani.
10 Ngozi yetu ina joto kama tanuru,
kutokana na fadhaa ya njaa.
11 Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni,
na mabikira katika miji ya Yuda.
12 Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao,
wazee hawapewi heshima.
13 Vijana wanataabika kwenye mawe ya kusagia,
wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni.
14 Wazee wameondoka katika lango la mji,
vijana wameacha kuimba nyimbo zao.
15 Furaha imeondoka mioyoni mwetu,
kucheza kwetu kumegeuka maombolezo.
16 Taji limeanguka kutoka kichwani petu.
Ole wetu, kwa maana tumetenda dhambi!
17 Kwa sababu hiyo, mioyo yetu inazimia,
kwa sababu ya hayo, macho yetu yamefifia,
18 kwa sababu Mlima Sayuni umekaa ukiwa,
na mbweha wanatembea juu yake.
 
19 Wewe, Ee Mwenyezi Mungu unatawala milele,
kiti chako cha enzi chadumu kizazi hadi kizazi.
20 Kwa nini watusahau siku zote?
Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu?
21 Turudishe kwako mwenyewe, Ee Mwenyezi Mungu,
ili tupate kurudi.
Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale,
22 isipokuwa uwe umetukataa kabisa
na umetukasirikia pasipo kipimo.