4
*Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.  1 Jinsi dhahabu ilivyopoteza mng’ao wake,  
dhahabu iliyo safi haing’ai!  
Vito vya thamani vimetawanywa  
kwenye mwanzo wa kila barabara.   
 2 Wana wa Sayuni wenye thamani,  
ambao mwanzo uzito wa thamani yao  
ulikuwa wa dhahabu,  
sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo,  
kazi ya mikono ya mfinyanzi!   
 3 Hata mbweha hutoa matiti yao  
kunyonyesha watoto wao,  
lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma  
kama mbuni jangwani.   
 4 Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga  
umegandamana na kaakaa la kinywa chake,  
watoto huomba mkate,  
lakini hakuna yeyote awapaye.   
 5 Wale waliokula vyakula vya kifahari  
ni maskini barabarani.  
Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau  
sasa wanalalia majivu.   
 6 Adhabu ya watu wangu  
ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,  
ambayo ilipinduliwa ghafula  
wala hapakuwa na mkono wa msaada.   
 7 Wakuu wao walikuwa wameng’aa kuliko theluji  
na weupe kuliko maziwa,  
miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,  
kuonekana kwao kama yakuti samawi.   
 8 Lakini sasa ni weusi kuliko masizi;  
hawatambulikani barabarani.  
Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,  
imekuwa mikavu kama fimbo.   
 9 Wale waliouawa kwa upanga ni bora  
kuliko wale wanaokufa njaa;  
wanateseka kwa njaa, wanatokomea  
kwa kukosa chakula kutoka shambani.   
 10 Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma  
wanapika watoto wao wenyewe,  
waliokuwa chakula chao  
watu wangu walipoangamizwa.   
 11 Mwenyezi Mungu ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;  
ameimwaga hasira yake kali.  
Amewasha moto katika Sayuni  
ambao umeteketeza misingi yake.   
 12 Wafalme wa dunia hawakuamini,  
wala mtu yeyote wa duniani,  
kwamba adui na watesi wangeweza kuingia  
kwenye malango ya Yerusalemu.   
 13 Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,  
na maovu ya makuhani wake,  
waliomwaga ndani yake  
damu ya wenye haki.   
 14 Sasa wanapapasa papasa barabarani  
kama watu ambao ni vipofu.  
Wamenajisiwa kabisa kwa damu,  
hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao.   
 15 Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!  
Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”  
Wanapokimbia na kutangatanga,  
watu miongoni mwa mataifa wanasema,  
“Hawawezi kukaa hapa zaidi.”   
 16 Mwenyezi Mungu mwenyewe amewatawanya;  
hawaangalii tena.  
Makuhani hawaoneshwi heshima,  
wazee hawakubaliki.   
 17 Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,  
kwa kutazamia bure msaada;  
tuliangalia kutoka minara yetu  
kwa taifa lisiloweza kutuokoa.   
 18 Watu walituvizia katika kila hatua  
hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu.  
Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,  
kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.   
 19 Waliotufuatia walikuwa wepesi  
kuliko tai angani;  
walitusaka juu milimani  
na kutuvizia jangwani.   
 20 Mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu, pumzi ya uhai wetu hasa,  
alinaswa katika mitego yao.  
Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake  
tungeishi miongoni mwa mataifa.   
 21 Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu,  
wewe unayeishi nchi ya Usi.  
Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,  
Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.   
 22 Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha,  
hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni.  
Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako,  
na atafunua uovu wako.   
*^ Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.