3
*Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.  1 Mimi ndiye mtu aliyeona mateso  
kwa fimbo ya ghadhabu yake.   
 2 Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee  
gizani wala si katika nuru;   
 3 hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu  
tena na tena, mchana kutwa.   
 4 Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa  
na ameivunja mifupa yangu.   
 5 Amenizingira na kunizunguka  
kwa uchungu na taabu.   
 6 Amenifanya niishi gizani  
kama wale waliokufa.   
 7 Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka,  
amenifunga kwa minyororo mizito.   
 8 Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada,  
anakataa kupokea maombi yangu.   
 9 Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe,  
amepotosha njia zangu.   
 10 Kama dubu aviziaye,  
kama simba mafichoni,   
 11 ameniburuta kutoka njiani,  
akanirarua na kuniacha bila msaada.   
 12 Amevuta upinde wake  
na kunifanya mimi niwe lengo kwa ajili ya mishale yake.   
 13 Alinichoma moyo wangu kwa mishale  
iliyotoka kwenye podo lake.   
 14 Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote,  
wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa.   
 15 Amenijaza kwa majani machungu  
na kunishibisha kwa nyongo.   
 16 Amevunja meno yangu kwa changarawe,  
amenikanyagia mavumbini.   
 17 Amani yangu imeondolewa,  
nimesahau kufanikiwa ni nini.   
 18 Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka  
na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu.”   
 19 Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu,  
uchungu na nyongo.   
 20 Ninayakumbuka vyema,  
nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.   
 21 Hata hivyo najikumbusha neno hili  
na kwa hiyo ninalo tumaini.   
 22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu, hatuangamii,  
kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.   
 23 Ni mpya kila asubuhi,  
uaminifu wako ni mkuu.   
 24 Nimeiambia nafsi yangu, “Mwenyezi Mungu ni fungu langu,  
kwa hiyo nitamngojea.”   
 25 Mwenyezi Mungu ni mwema kwa wale wanaomtumaini,  
na kwa yule anayemtafuta;   
 26 ni vyema kungojea kwa utulivu  
kwa ajili ya wokovu wa Mwenyezi Mungu.   
 27 Ni vyema mtu kuchukua nira  
bado angali kijana.   
 28 Na akae peke yake awe kimya,  
kwa maana Mwenyezi Mungu ameiweka juu yake.   
 29 Hata azike uso wake mavumbini  
bado tumaini litakuwepo.   
 30 Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye,  
na ajazwe na aibu.   
 31 Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali  
na Bwana milele.   
 32 Ingawa huleta huzuni, ataonesha huruma,  
kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.   
 33 Kwa maana hapendi kuwaletea mateso  
au huzuni watoto wa wanadamu.   
 34 Kuwaponda chini ya nyayo  
wafungwa wote katika nchi,   
 35 Kumnyima mtu haki zake  
mbele za Aliye Juu Sana,   
 36 kumnyima mtu haki:  
Je, Bwana asione mambo kama haya?   
 37 Nani awezaye kusema nalo likatendeka  
kama Bwana hajaamuru?   
 38 Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana  
ndiko yatokako maafa na mambo mema?   
 39 Je, mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika  
wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake?   
 40 Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu,  
na tumrudie Mwenyezi Mungu.   
 41 Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu  
kwa Mungu mbinguni, na tuseme:   
 42 “Tumetenda dhambi na kuasi  
nawe hujasamehe.   
 43 “Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia;  
umetuchinja bila huruma.   
 44 Unajifunika mwenyewe kwa wingu,  
ili pasiwe na ombi  
litakaloweza kupenya.   
 45 Umetufanya takataka na uchafu  
miongoni mwa mataifa.   
 46 “Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao  
wazi dhidi yetu.   
 47 Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula,  
uharibifu na maangamizi.”   
 48 Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu,  
kwa sababu watu wangu wameangamizwa.   
 49 Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma,  
bila kupata nafuu,   
 50 hadi Mwenyezi Mungu atazame chini  
kutoka mbinguni na kuona.   
 51 Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini  
kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu.   
 52 Wale waliokuwa adui zangu bila sababu  
wameniwinda kama ndege.   
 53 Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo  
na kunitupia mawe;   
 54 maji yalifunika juu ya kichwa changu,  
nami nikafikiri nilikuwa karibu  
kukatiliwa mbali.   
 55 Nililiitia jina lako, Ee Mwenyezi Mungu,  
kutoka vina vya shimo.   
 56 Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako  
kilio changu nikuombapo msaada.”   
 57 Ulikuja karibu nilipokuita,  
nawe ukasema, “Usiogope.”   
 58 Ee Bwana, ulichukua shauri langu,  
ukaukomboa uhai wangu.   
 59 Umeona, Ee Mwenyezi Mungu, ubaya niliotendewa.  
Tetea shauri langu!   
 60 Umeona kina cha kisasi chao,  
mashauri yao yote mabaya dhidi yangu.   
 61 Ee Mwenyezi Mungu, umesikia matukano yao,  
mashauri yao yote mabaya dhidi yangu:   
 62 kile adui zangu wanachonong’ona na kunung’unikia  
dhidi yangu mchana kutwa.   
 63 Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama,  
wananidhihaki katika nyimbo zao.   
 64 Uwalipe kile wanachostahili, Ee Mwenyezi Mungu,  
kwa yale ambayo mikono yao imetenda.   
 65 Weka pazia juu ya mioyo yao,  
laana yako na iwe juu yao!   
 66 Wafuatilie katika hasira na uwaangamize  
chini ya mbingu za Mwenyezi Mungu.   
*^ Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.