2
*Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.  1 Tazama jinsi Bwana alivyomfunika Binti Sayuni  
kwa wingu la hasira yake!  
Ameitupa chini fahari ya Israeli  
kutoka mbinguni hadi duniani,  
hakukumbuka kiti chake cha kuwekea miguu  
katika siku ya hasira yake.   
 2 Bila huruma Bwana ameyameza  
makao yote ya Yakobo;  
katika ghadhabu yake amebomoa  
ngome za Binti Yuda.  
Ameuangusha ufalme wake na wakuu wake  
chini kwa aibu.   
 3 Katika hasira kali amevunja  
kila pembe†pembe inawakilisha nguvu; pia 2:17 ya Israeli.  
Ameuondoa mkono wake wa kuume  
alipokaribia adui.  
Amemteketeza Yakobo kama moto uwakao  
ule uteketezao kila kitu kinachouzunguka.   
 4 Ameupinda upinde wake kama adui,  
mkono wake wa kuume uko tayari.  
Kama vile adui amewaua  
wote waliokuwa wanapendeza jicho,  
amemwaga ghadhabu yake kama moto  
juu ya hema la Binti Sayuni.   
 5 Bwana ni kama adui;  
amemmeza Israeli.  
Ameyameza majumba yake yote ya kifalme  
na kuangamiza ngome zake.  
Ameongeza huzuni na maombolezo  
kwa Binti Yuda.   
 6 Ameharibu maskani yake kama bustani,  
ameharibu mahali pake pa mkutano.  
Mwenyezi Mungu amemfanya Sayuni kusahau  
sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake;  
katika hasira yake kali amewadharau  
mfalme na kuhani.   
 7 Bwana amekataa madhabahu yake  
na kuacha mahali patakatifu pake.  
Amemkabidhi adui kuta  
za majumba yake ya kifalme;  
wameshangilia katika nyumba ya Mwenyezi Mungu  
kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa.   
 8 Mwenyezi Mungu alikusudia kuangusha  
ukuta uliomzunguka Binti Sayuni.  
Ameinyoosha kamba ya kupimia  
na hakuuzuia mkono wake usiangamize.  
Alifanya maboma na kuta ziomboleze,  
vyote vikaharibika pamoja.   
 9 Malango yake yamezama ardhini,  
makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu.  
Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni  
miongoni mwa mataifa,  
sheria haipo tena,  
na manabii wake hawapati tena  
maono kutoka kwa Mwenyezi Mungu.   
 10 Wazee wa Binti Sayuni  
wanaketi chini kimya,  
wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao  
na kuvaa gunia.  
Wanawali wa Yerusalemu  
wameinamisha vichwa vyao hadi chini.   
 11 Macho yangu yamedhoofika kwa kulia,  
nina maumivu makali ndani,  
moyo wangu umemiminwa ardhini  
kwa sababu watu wangu wameangamizwa,  
kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia  
kwenye barabara za mji.   
 12 Wanawaambia mama zao,  
“Wapi mkate na divai?”  
wazimiapo kama watu waliojeruhiwa  
katika barabara za mji,  
maisha yao yadhoofikavyo  
mikononi mwa mama zao.   
 13 Ninaweza kusema nini kwa ajili yako?  
Nikulinganishe na nini,  
ee Binti Yerusalemu?  
Nitakufananisha na nini,  
ili nipate kukufariji,  
ee Bikira Binti Sayuni?  
Jeraha lako lina kina kama bahari.  
Ni nani awezaye kukuponya?   
 14 Maono ya manabii wako  
yalikuwa ya uongo na yasiyofaa kitu,  
hawakuifunua dhambi yako  
ili kukuzuilia kwenda utumwani.  
Maneno waliyokupa  
yalikuwa ya uongo na ya kupotosha.   
 15 Wote wapitiao njia yako  
wanakupigia makofi,  
wanakudhihaki na kutikisa vichwa vyao  
kwa Binti Yerusalemu:  
“Huu ndio ule mji ulioitwa  
mkamilifu wa uzuri,  
furaha ya dunia yote?”   
 16 Adui zako wote wanapanua  
vinywa vyao dhidi yako,  
wanadhihaki na kusaga meno yao  
na kusema, “Tumemmeza.  
Hii ndiyo siku tuliyoingojea,  
tumeishi na kuiona.”   
 17 Mwenyezi Mungu amefanya lile alilolipanga;  
ametimiza neno lake  
aliloliamuru siku za kale.  
Amekuangusha bila huruma,  
amewaacha adui wakusimange,  
ametukuza pembe ya adui yako.   
 18 Mioyo ya watu  
inamlilia Bwana.  
Ee ukuta wa Binti Sayuni,  
machozi yako na yatiririke kama mto  
usiku na mchana;  
usijipe nafuu,  
macho yako yasipumzike.   
 19 Inuka, lia usiku,  
zamu za usiku zianzapo;  
mimina moyo wako kama maji  
mbele za Bwana.  
Mwinulie yeye mikono yako  
kwa ajili ya maisha ya watoto wako,  
ambao wanazimia kwa njaa  
kwenye kila mwanzo wa barabara.   
 20 “Tazama, Ee Mwenyezi Mungu, ufikirie:  
Ni nani ambaye umepata kumtendea namna hii?  
Je, wanawake wale wazao wao,  
watoto waliowalea?  
Je, kuhani na nabii auawe  
mahali patakatifu pa Bwana?   
 21 “Vijana na wazee hujilaza pamoja  
katika mavumbi ya barabarani,  
wasichana wangu na wavulana wangu  
wameanguka kwa upanga.  
Umewaua katika siku ya hasira yako,  
umewachinja bila huruma.   
 22 “Kama ulivyoita siku ya karamu,  
ndivyo ulivyoagiza mapigo dhidi yangu kila upande.  
Katika siku ya hasira ya Mwenyezi Mungu  
hakuna yeyote aliyekwepa au kupona;  
wale niliowatunza na kuwalea,  
adui yangu amewaangamiza.”