21
Kuzaliwa kwa Isaka
Wakati huu Mwenyezi Mungu akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, na Mwenyezi Mungu akamtendea Sara kama alivyoahidi. Sara akapata mimba, na akamzalia Ibrahimu mwana katika uzee wake, katika majira yale Mungu alikuwa amemwahidi. Ibrahimu akampa huyo mwana ambaye Sara alimzalia jina Isaka*maana yake Kicheko au Anacheka. Isaka alipokuwa na umri wa siku nane, Ibrahimu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru. Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka mia moja Isaka mwanawe alipozaliwa.
Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, na kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.” Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Ibrahimu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Lakini nimemzalia mwana katika uzee wake.”
Hajiri na Ishmaeli wafukuzwa
Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya. Siku ile Isaka aliyoachishwa kunyonya, Ibrahimu alifanya sherehe kubwa. Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hajiri Mmisri alimzalia Ibrahimu alikuwa anadhihaki. 10 Hivyo Sara akamwambia Ibrahimu, “Mwondoe mjakazi huyu mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mjakazi huyo kamwe hatarithi na mwanangu Isaka.”
11 Jambo hili lilimhuzunisha sana Ibrahimu kwa sababu lilimhusu mwanawe. 12 Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana huyo na mjakazi wako. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka. 13 Nitamfanya huyu mwana wa mjakazi wako kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”
14 Kesho yake asubuhi na mapema, Ibrahimu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hajiri. Akaviweka begani mwa Hajiri, akamwondoa pamoja na kijana. Hajiri akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.
15 Maji yalipokwisha kwenye kiriba, Hajiri akamwacha kijana chini ya kichaka. 16 Kisha akaenda akaketi kama umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Akiwa ameketi pale, akaanza kulia kwa huzuni.
17 Mungu akamsikia kijana akilia. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini, Hajiri? Usiogope, Mungu amesikia kijana akilia akiwa amelala pale. 18 Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”
19 Ndipo Mungu akamfumbua Hajiri macho, akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.
20 Mungu akawa pamoja na huyo kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde. 21 Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akamtwalia mke kutoka Misri.
Mapatano katika Beer-Sheba
22 Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Ibrahimu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. 23 Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”
24 Ibrahimu akasema, “Ninaapa hivyo.”
25 Ndipo Ibrahimu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyang’anya. 26 Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ametenda hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”
27 Hivyo Ibrahimu akaleta kondoo na ng’ombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano. 28 Ibrahimu akatenga kondoo jike saba kutoka kwa kundi. 29 Abimeleki akamuuliza Ibrahimu, “Ni nini maana ya hawa kondoo jike saba uliowatenga peke yao?”
30 Ibrahimu akamjibu, “Pokea hawa kondoo jike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”
31 Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu hao wawili waliapiana hapo.
32 Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi nchi ya Wafilisti. 33 Ibrahimu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa milele. 34 Naye Ibrahimu akakaa nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.

*21:3 maana yake Kicheko au Anacheka