22
Kujua uthabiti wa Ibrahimu
Baadaye Mungu akamjaribu Ibrahimu. Akamwambia, “Ibrahimu!”
Ibrahimu akamjibu, “Mimi hapa.”
Kisha Mungu akamwambia, “Mchukue mwanao, mwana wako wa pekee umpendaye, Isaka, uende nchi ya Moria. Mtoe kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima nitakaokuambia.”
Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia. Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali. Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunaenda kule. Tutaabudu na kisha tutawarudia.”
Ibrahimu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaka mwanawe, naye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, Isaka akamwambia Ibrahimu baba yake, “Baba yangu!”
Ibrahimu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.”
Isaka akasema, “Moto na kuni zipo. Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”
Ibrahimu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.
Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. 10 Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe. 11 Lakini malaika wa Mwenyezi Mungu akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Ibrahimu! Ibrahimu!”
Akajibu, “Mimi hapa.”
12 Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”
13 Ibrahimu akainua macho, akaona nyuma yake kondoo dume akiwa amenaswa pembe zake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14 Ibrahimu akapaita mahali pale Yehova-Yire.*maana yake Mwenyezi Mungu atapata Hadi leo inasemekana, “Katika mlima wa Mwenyezi Mungu itapatikana.”
15 Basi malaika wa Mwenyezi Mungu akamwita Ibrahimu kutoka mbinguni mara ya pili, 16 akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Mwenyezi Mungu, kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee: 17 Hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga wa pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, 18 na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”
19 Ndipo Ibrahimu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wote, wakaenda hadi Beer-Sheba. Naye Ibrahimu akaishi huko Beer-Sheba.
Wana wa Nahori
20 Baada ya muda, Ibrahimu akaambiwa, “Milka pia amepata watoto; amemzalia ndugu yako Nahori wana:
21 Usi mzaliwa wake wa kwanza, Buzi nduguye,
Kemueli (baba wa Aramu),
22 Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.”
23 Bethueli akamzaa Rebeka.
Milka alimzalia Nahori nduguye Ibrahimu hao wana wanane.
 
24 Suria wake Nahori aliyeitwa Reuma pia alizaa wana:
Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.

*22:14 maana yake Mwenyezi Mungu atapata