23
Kifo cha Sara
Sara aliishi miaka mia moja na ishirini na saba (127). Sara akafa huko Kiriath-Arba (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani, naye Ibrahimu akalia na kumwomboleza Sara.
Ndipo Ibrahimu akainuka kutoka pale penye maiti ya mke wake. Akazungumza na Wahiti, akasema, “Mimi ni mpitaji na mgeni miongoni mwenu. Niuzieni sehemu ya ardhi yenu ili niweze kumzika maiti wangu.”
Wahiti wakamjibu Ibrahimu, “Bwana, tusikilize. Wewe ni mtawala mkuu sana miongoni mwetu. Zika maiti wako katika kaburi unalolipenda kati ya makaburi yetu. Hakuna mtu wa kwetu atakayekuzuia kaburi lake ili kuzika maiti wako.”
Ibrahimu akainuka, akasujudu mbele ya Wahiti, wenyeji wa nchi hiyo. Akawaambia, “Kama mnaniruhusu kumzika maiti wangu, basi nisikilizeni, mkamsihi Efroni mwana wa Sohari kwa niaba yangu ili aniuzie pango la Makpela, lililo mali yake, nalo liko mwisho wa shamba lake. Mwambieni aniuzie kwa bei kamili atakayosema ili liwe mahali pangu pa kuzikia miongoni mwenu.”
10 Efroni Mhiti alikuwa ameketi miongoni mwa watu wake; akamjibu Ibrahimu mbele ya Wahiti wote waliokuwa katika lango la mji: 11 “La, bwana wangu, nisikilize. Nakupa shamba, na pia nakupa pango lililo ndani yake. Nakupa mbele ya watu wangu, uzike maiti wako.”
12 Ibrahimu akasujudu tena mbele ya wenyeji wa nchi, 13 akamwambia Efroni wale watu wakiwa wanasikia, “Tafadhali nisikilize. Nitakulipa fedha za hilo shamba. Kubali kuzipokea ili niweze kumzika maiti wangu.”
14 Efroni akamjibu Ibrahimu, 15 “Nisikilize, bwana wangu, thamani ya ardhi hiyo ni shekeli mia nne za fedha*Shekeli 400 za fedha ni sawa na kilo 4.5., lakini hiyo ni nini kati yako na mimi? Mzike maiti wako.”
16 Ibrahimu akakubali masharti ya Efroni, akampimia ile fedha aliyotaja masikioni mwa Wahiti: shekeli mia nne za fedha kulingana na viwango vya uzito vilivyokuwa vikitumika wakati huo na wafanyabiashara.
17 Hivyo shamba la Efroni huko Makpela karibu na Mamre, yaani shamba pamoja na pango lililokuwamo, nayo miti yote iliyokuwa ndani ya mipaka ya shamba hilo, vilikabidhiwa 18 kwa Ibrahimu kuwa mali yake mbele ya Wahiti wote waliokuwa wamekuja kwenye lango la mji. 19 Baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe kwenye pango ndani ya shamba la Makpela karibu na Mamre (huko Hebroni) katika nchi ya Kanaani. 20 Hivyo Wahiti wakamkabidhi Ibrahimu shamba pamoja na pango lililokuwa humo kuwa mahali pa kuzikia.

*23:15 Shekeli 400 za fedha ni sawa na kilo 4.5.