27
Isaka ambariki Yakobo
1 Isaka alipokuwa mzee na macho yake yakapofuka kwa kukosa nguvu, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.”
Akajibu, “Mimi hapa.”
2 Isaka akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kufa kwangu. 3 Sasa basi chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukaniwindie mawindo. 4 Uniandalie chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili nikubariki kabla sijafa.”
5 Rebeka alikuwa akisikiliza Isaka akizungumza na mwanawe Esau. Basi Esau alipoenda nyikani kuwinda mawindo ayalete, 6 Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau, 7 ‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili nikubariki mbele za Mwenyezi Mungu kabla sijafa.’ 8 Sasa mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia: 9 Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili nimwandalie baba yako chakula kitamu kile anachokipenda. 10 Kisha umpelekee baba yako ale, ili akubariki kabla hajafa.”
11 Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, nami nina ngozi nyororo. 12 Itakuwaje baba yangu akinigusa? Ataona kama ninamfanyia ujanja, nami nijiletee laana badala ya baraka.”
13 Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia: nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.”
14 Kwa hiyo alienda akawaleta, akampa mama yake, naye Rebeka akaandaa chakula kitamu, kile alichokipenda baba yake. 15 Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. 16 Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi. 17 Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.
18 Yakobo akaenda kwa baba yake, akasema, “Baba yangu.”
Akajibu, “Naam, mwanangu. Wewe ni nani?”
19 Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili unibariki.”
20 Isaka akamuuliza mwanawe, “Umepataje mawindo haraka hivi, mwanangu?”
Akajibu, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.”
21 Kisha Isaka akamwambia Yakobo, “Mwanangu, tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.”
22 Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaka, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.” 23 Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki. 24 Akamuuliza, “Kweli wewe ni mwanangu Esau?”
Akajibu, “Ni mimi.”
25 Kisha Isaka akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nikubariki.”
Yakobo akamletea, naye akala; kisha akamletea na divai akanywa. 26 Ndipo Isaka baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.”
27 Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaka aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema,
“Aha, harufu ya mwanangu
ni kama harufu ya shamba
ambalo Mwenyezi Mungu amelibariki.
28 Mungu na akupe umande wa mbinguni
na utajiri wa duniani:
wingi wa nafaka na divai mpya.
29 Mataifa yakutumikie,
na mataifa yakusujudie.
Uwe bwana juu ya ndugu zako,
na wana wa mama yako wakusujudie.
Walaaniwe wale wanaokulaani,
na wabarikiwe wale wanaokubariki.”
30 Baada ya Isaka kumbariki Yakobo, na punde tu alipoondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni. 31 Naye pia akaandaa chakula kitamu, akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.”
32 Isaka baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?”
Akamjibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.”
33 Isaka akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!”
34 Esau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia kwa sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki! Nibariki mimi pia, baba yangu!”
35 Lakini akamjibu, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu, akachukua baraka yako.”
36 Esau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?”
37 Isaka akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako; pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, na nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?”
38 Esau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa.
39 Baba yake Isaka akamjibu,
“Makao yako yatakuwa
mbali na utajiri wa dunia,
mbali na umande wa mbinguni.
40 Utaishi kwa upanga,
nawe utamtumikia ndugu yako.
Lakini utakapokuwa umejikomboa,
utatupa nira yake
kutoka shingoni mwako.”
41 Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia; ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”
42 Rebeka alipoambiwa yale Esau mwanawe mkubwa aliyoyasema, akamtumania Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua. 43 Sasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani. 44 Ukae naye kwa muda hadi ghadhabu ya ndugu yako itulie. 45 Ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze nyote wawili siku moja?”
46 Kisha Rebeka akamwambia Isaka, “Nimechukia maisha kwa sababu ya hawa wanawake Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mke miongoni mwa wanawake wa nchi hii, wanawake Wahiti kama hawa, sitaona haja ya kuendelea kuishi.”