30
1 Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea dada yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!”
2 Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia kuzaa watoto?”
3 Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mjakazi wangu. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto, na kupitia kwake mimi pia niweze kuwa na uzao.”
4 Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili, 5 naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. 6 Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu; amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa hiyo akamwita jina Dani*maana yake Anahukumu.
7 Bilha mjakazi wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. 8 Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita jina Naftali†maana yake Nimeshindana.
9 Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mjakazi wake Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake. 10 Zilpa mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana. 11 Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita jina Gadi‡maana yake Jeshi laja.
12 Mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili. 13 Ndipo Lea akasema, “Nina furaha kiasi gani! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita jina Asheri§maana yake Nimefurahi.
14 Msimu wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akachuma tunguja ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
15 Lakini Lea akamwambia, “Haikukutosha kuninyang’anya mume wangu? Je, utachukua na tunguja za mwanangu pia?”
Raheli akasema, “Vema sana! Yakobo atakutana nawe kimwili leo usiku, kwa malipo ya tunguja za mwanao.”
16 Kwa hiyo Yakobo alipokuja kutoka shambani jioni ile, Lea akaenda kumlaki, akamwambia, “Lazima ukutane nami kimwili. Nimekukodisha kwa tunguja za mwanangu.” Kwa hiyo akakutana naye kimwili usiku ule.
17 Mungu akamsikiliza Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano. 18 Ndipo Lea akasema, “Mungu amenizawadia kwa kumpa mume wangu mjakazi wangu.” Kwa hiyo akamwita jina Isakari*maana yake Zawadi.
19 Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa sita. 20 Ndipo Lea aliposema, “Mungu amenizawadia kwa zawadi ya thamani sana. Sasa mume wangu ataniheshimu kwa sababu nimemzalia wana sita.” Kwa hiyo akamwita jina Zabuloni†maana yake Heshima.
21 Baadaye akamzaa mtoto wa kike, akamwita jina Dina‡maana yake Tetea haki.
22 Ndipo Mungu akamkumbuka Raheli, akasikia maombi yake na akafungua tumbo lake. 23 Akapata mimba na akamzaa mwana; akasema, “Mungu ameniondolea aibu yangu.”
24 Akamwita jina Yusufu§maana yake Yeye na aongeze, akasema, “Mwenyezi Mungu na anipe mwana mwingine.”
Makundi ya Yakobo yaongezeka
25 Baada ya Raheli kumzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, “Nipe ruhusa nirudi katika nchi yangu. 26 Nipe wake zangu na watoto, ambao nimetumika kuwapata, nami niende zangu. Unajua kazi niliyokufanyia.”
27 Lakini Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, tafadhali ukae. Nimegundua kwa uaguzi kwamba Mwenyezi Mungu amenibariki kwa sababu yako.” 28 Akaongeza kumwambia, “Taja ujira wako nami nitakulipa.”
29 Yakobo akamwambia, “Unajua jinsi nimekutumikia na jinsi wanyama wako walivyolishwa vizuri chini ya uangalizi wangu. 30 Kidogo ulichokuwa nacho kabla sijaja kimeongezeka sana, naye Mwenyezi Mungu amekubariki popote nilipokuwa. Lakini sasa, ni lini nitashughulikia mambo ya nyumba yangu mwenyewe?”
31 Labani akamuuliza, “Nikupe nini?”
Yakobo akamjibu, “Usinipe chochote, lakini kama utanifanyia jambo hili moja, nitaendelea kuchunga na kuyaangalia makundi yako. 32 Niruhusu nipite katika makundi yako yote leo niondoe humo kila kondoo mwenye mabaka mabaka au madoadoa, kila mwana-kondoo mweusi, na kila mbuzi mwenye madoadoa au mabaka mabaka. Hawa watakuwa ujira wangu. 33 Uadilifu wangu utanishuhudia siku zijazo, kila utakapochunguza ujira ambao umenilipa mimi. Mbuzi yeyote wangu ambaye hana mabaka mabaka wala madoadoa, au mwana-kondoo ambaye si mweusi, atahesabika ameibwa.”
34 Labani akasema, “Ninakubali; na iwe kama ulivyosema.” 35 Siku ile ile Yakobo akawaondoa beberu wote waliokuwa na mistari au madoadoa, na mbuzi jike wote waliokuwa na mistari au madoadoa (wote waliokuwa na alama nyeupe juu yao), na wana-kondoo weusi wote, akawaweka chini ya uangalizi wa wanawe. 36 Kisha Labani akamwacha Yakobo kwa mwendo wa safari ya siku tatu, naye Yakobo akaendelea kuchunga lile kundi la Labani lililobaki.
37 Lakini Yakobo akachukua fito mbichi zilizokatwa wakati huo huo za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni, akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo. 38 Kisha akaweka fito hizo katika mabirika yote ya kunyweshea mifugo, ili ziwe mbele ya makundi walipokuja kunywa maji. Wanyama walipokuja kunywa maji, hali wakiwa wanahitaji mbegu, 39 wakapandwa hizo fito zikiwa mbele yao. Wanyama waliopata mimba mbele ya hizo fito walizaa wanyama wenye mistari, madoadoa na mabaka mabaka. 40 Yakobo akawatenga wadogo wa kundi peke yao, lakini akazielekeza nyuso za hao waliobaki kwenye wale wenye mistari na weusi waliokuwa mali ya Labani. Hivyo akatenga makundi yake mwenyewe, wala hakuwachanganya na wanyama wa Labani. 41 Kila mara wanyama wenye nguvu walipohitaji mbegu, Yakobo aliweka zile fito kwenye mabirika mbele ya hao wanyama, ili wapandwe karibu na hizo fito, 42 lakini ikiwa wanyama walikuwa wadhaifu hakuziweka hizo fito. Hivyo wanyama wadhaifu wakawa wa Labani, na wanyama wenye nguvu wakawa wa Yakobo. 43 Hivyo Yakobo akastawi sana, tena akawa na makundi makubwa, mjakazi na watumishi, na ngamia na punda.