31
Yakobo akimbia kutoka kwa Labani
1 Yakobo akawasikia wana wa Labani wakisema, “Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu, naye amepata utajiri huu wote kutokana na mali ya baba yetu.” 2 Yakobo akatambua kwamba moyo wa Labani kwake umebadilika.
3 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.”
4 Hivyo Yakobo akatuma ujumbe kwa Raheli na Lea waje malishoni kwenye makundi yake. 5 Akawaambia, “Naona moyo wa baba yenu kwangu umebadilika, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. 6 Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote, 7 lakini baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru. 8 Aliposema, ‘Wenye madoadoa watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye madoadoa. Aliposema, ‘Wenye mistari watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye mistari. 9 Hivyo Mungu amechukua mifugo ya baba yenu na amenipa mimi.
10 “Majira ya kuzaliana niliota ndoto. Niliinua macho na kuona kwamba wale beberu waliokuwa wakiwapanda mbuzi walikuwa wana mistari, madoadoa na mabaka mabaka. 11 Malaika wa Mungu akaniita katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’ 12 Akaniambia, ‘Inua macho yako uone wale beberu wote wanaowapanda mbuzi wana mistari, madoadoa au mabaka mabaka, kwa maana nimeona yale yote Labani amekutendea. 13 Mimi ndiye Mungu wa Betheli, ulikomiminia nguzo mafuta, na ukaniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii mara moja urudi katika nchi uliyozaliwa.’ ”
14 Ndipo Raheli na Lea wakajibu, “Je bado tunalo fungu lolote katika urithi wa nyumba ya baba yetu? 15 Je, yeye hatuhesabu sisi kama wageni? Sio kwamba ametuuza tu, bali ametumia hata mali tuliyolipiwa. 16 Hakika utajiri wote ambao Mungu ameuchukua kutoka kwa baba yetu ni mali yetu na watoto wetu. Hivyo fanya lolote lile Mungu alilokuambia.”
17 Ndipo Yakobo akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia. 18 Naye akawaswaga wanyama wote mbele yake, pamoja na mali yote aliyokuwa amepata huko Padan-Aramu ili aende kwa baba yake Isaka katika nchi ya Kanaani.
19 Labani alipokuwa ameenda kukata kondoo wake manyoya, Raheli aliiba miungu ya nyumbani mwa baba yake. 20 Zaidi ya hayo, Yakobo alimdanganya Labani Mwaramu*au Mshami kwa kutokumwambia kwamba anakimbia. 21 Hivyo akakimbia pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo na kuvuka Mto†yaani Mto Frati, akaelekea nchi ya vilima ya Gileadi.
Labani amfuatilia Yakobo
22 Siku ya tatu, Labani akaambiwa kwamba Yakobo amekimbia. 23 Akiwachukua jamaa zake, akamfuatia Yakobo kwa siku saba na kumkuta kwenye nchi ya vilima ya Gileadi. 24 Ndipo Mungu akamjia Labani Mwaramu katika ndoto usiku na kumwambia, “Jihadhari usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.”
25 Yakobo alikuwa amepiga hema lake katika nchi ya vilima ya Gileadi wakati Labani alimfikia; naye Labani na jamaa yake wakapiga kambi huko pia. 26 Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Umenidanganya na umewachukua binti zangu kama mateka katika vita. 27 Kwa nini ulikimbia kwa siri na kunidanganya? Kwa nini hukuniambia ili nikuage kwa furaha na nyimbo za matari na vinubi? 28 Hata hukuniruhusu niwabusu wajukuu zangu na kuwaaga binti zangu. Umefanya kitu cha kipumbavu. 29 Nina uwezo wa kukudhuru, lakini usiku uliopita Mungu wa baba yako alisema nami, akaniambia, ‘Jihadhari, usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.’ 30 Sasa umeondoka kwa sababu umetamani kurudi nyumbani mwa baba yako. Lakini kwa nini umeiiba miungu yangu?”
31 Yakobo akamjibu Labani, “Niliogopa, kwa sababu nilifikiri ungeweza kuninyang’anya binti zako kwa nguvu. 32 Lakini ukimkuta yeyote na miungu yako, huyo mtu hataishi. Mbele ya jamaa zetu, angalia mwenyewe uone kama kuna chochote chako hapa nilicho nacho; kama kipo, kichukue.” Basi Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiiba hiyo miungu.
33 Kwa hiyo Labani akaingia ndani ya hema la Yakobo, na ndani ya hema la Lea, na ndani ya hema la wajakazi wale wawili, lakini hakuipata hiyo miungu. Baadaye alipotoka hema la Lea, akaingia hema la Raheli. 34 Basi Raheli ndiye alikuwa ameichukua ile miungu ya nyumbani mwao na kuiweka katika matandiko ya ngamia, na kukalia. Labani akatafuta kila mahali kwenye hema lakini hakupata chochote.
35 Raheli akamwambia baba yake, “Usikasirike bwana wangu, kwa kuwa siwezi kusimama ukiwepo, niko katika hedhi.” Labani akatafuta lakini hakuweza kuipata miungu ya nyumbani mwake.
36 Yakobo akakasirika na kumshutumu Labani, akisema, “Uhalifu wangu ni nini?” Akamuuliza Labani, “Ni dhambi gani niliyofanya hata unaniwinda? 37 Sasa kwa kuwa umepekua vitu vyangu vyote, umepata nini kilicho cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya jamaa yako na yangu, nao waamue kati yetu.
38 “Hadi sasa nimekuwa pamoja nawe miaka ishirini. Kondoo wako na mbuzi wako hawajaharibu mimba, wala sijala kondoo dume kutoka makundi yako. 39 Sijakuletea mfugo aliyeraruliwa na wanyama pori, bali nimegharimia hasara mwenyewe. Tena umenidai malipo kwa chochote kilichoibwa mchana au usiku. 40 Hali yangu imekuwa hivi: Nimechomwa kwa joto la mchana, na kupigwa na baridi usiku, pia usingizi ulinipotea. 41 Imekuwa hivi kwa miaka ile ishirini niliyokuwa nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka ile kumi na nne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita kwa ajili ya makundi yako, nawe ulibadilisha ujira wangu mara kumi. 42 Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hakuwa pamoja nami, hakika ungenifukuza mikono mitupu. Lakini Mungu ameona taabu yangu na kazi ngumu ya mikono yangu, naye usiku uliopita amekukemea.”
43 Labani akamjibu Yakobo, “Wanawake hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu, na makundi haya ni makundi yangu. Vyote unavyoviona ni vyangu. Lakini hata hivyo ninaweza kufanya nini kuhusu hawa binti zangu, au kuhusu watoto waliowazaa? 44 Njoo sasa na tufanye agano, wewe na mimi, na liwe kama shahidi kati yetu.”
45 Hivyo Yakobo akachukua jiwe, akalisimamisha kama nguzo. 46 Akawaambia jamaa yake, “Kusanyeni mawe.” Hivyo wakachukua mawe na kuyakusanya yakawa lundo; wakala chakula hapo karibu na hilo lundo. 47 Labani akaliita Yegar-Sahadutha‡maana yake Lundo la ushahidi kwa Kiaramu na Yakobo akaliita Galeedi.§maana yake Lundo la ushahidi kwa Kiebrania
48 Labani akasema, “Lundo hili ni shahidi kati yako na mimi leo.” Ndiyo maana likaitwa Galeedi. 49 Pia liliitwa Mispa*maana yake Mnara wa ulinzi, kwa sababu alisema, “Mwenyezi Mungu na aweke ulinzi kati yako na mimi wakati hatuko pamoja. 50 Ukiwatenda mabaya binti zangu au ukioa wake wengine zaidi ya binti zangu, hata ingawa hakuna hata mmoja aliye pamoja nasi, kumbuka kwamba Mungu ni shahidi kati yako na mimi.”
51 Pia Labani akamwambia Yakobo, “Hili ndilo lundo, na hii ndiyo nguzo niliyoisimamisha kati yako na mimi. 52 Lundo hili ni shahidi na nguzo hii ni shahidi, kwamba sitavuka lundo hili kuja upande wako kukudhuru, nawe kwamba hutavuka lundo hili na nguzo hii kuja upande wangu kunidhuru. 53 Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba zao, aamue kati yetu.”
Hivyo Yakobo akaapa kwa jina la Hofu ya baba yake Isaka. 54 Yakobo akatoa dhabihu huko nchi ya vilima na akawaalika jamaa zake kula chakula. Baada ya kula, wakalala huko.
55 Kesho yake asubuhi na mapema, Labani akawabusu wajukuu zake na binti zake, na kuwabariki. Kisha akaondoka, akarudi nyumbani.