32
Yakobo ajiandaa kukutana na Esau
1 Yakobo pia akaondoka akaenda zake, nao malaika wa Mungu wakakutana naye. 2 Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu*maana yake Kambi mbili.
3 Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu. 4 Akawaagiza, akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema: nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwa huko hadi sasa. 5 Ninao ng’ombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’ ”
6 Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulienda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume mia nne.”
7 Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili; pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vilevile ng’ombe na ngamia. 8 Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litanusurika.”
9 Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, Mungu wa baba yangu Isaka, Ee Mwenyezi Mungu, ndiwe uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi.’ 10 Sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi, mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa nimekuwa makundi mawili. 11 Nakuomba uniokoe kutoka kwa mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia kina mama pamoja na watoto wao. 12 Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’ ”
13 Akalala pale usiku ule. Miongoni mwa vitu alivyokuwa navyo, akachagua zawadi kwa ajili ya Esau ndugu yake: 14 beberu ishirini na mbuzi jike mia mbili, kondoo dume ishirini na kondoo jike mia mbili, 15 ngamia jike thelathini pamoja na ndama zao, ng’ombe arobaini na mafahali kumi, punda jike ishirini, na punda wa kiume kumi. 16 Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake, na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.”
17 Akamwagiza yule aliyetangulia hivi, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unaenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’ 18 utamjibu hivi, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi iliyotumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ”
19 Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, na wa kundi la tatu, na kila mtumishi wa yale mengine yaliyofuata, hivi: “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye. 20 Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza; hatimaye nitakapomwona, huenda atanikubali.” 21 Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.
Yakobo amenyana na Mungu
22 Usiku ule Yakobo akaamka, akawachukua wake zake wawili, wajakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Mto Yaboki. 23 Baada ya kuwavusha ng’ambo ya kijito, alivusha pia mali yake yote. 24 Kwa hiyo Yakobo akaachwa peke yake; naye mtu mmoja akashikana naye mweleka hadi mapambazuko. 25 Yule mtu alipoona kuwa hawezi kumshinda, aligusa kiungio cha nyonga ya Yakobo; kwa hiyo nyonga yake ikateguka alipokuwa akishikana mweleka na yule mtu. 26 Ndipo yule mtu akasema, “Niache niende, kwa kuwa ni mapambazuko.”
Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”
27 Yule mtu akamuuliza, “Jina lako ni nani?”
Akamjibu, “Ni Yakobo.”
28 Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli†maana yake Yeye ashindanaye na Mungu, kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia, nawe umeshinda.”
29 Yakobo akasema, “Tafadhali niambie jina lako.”
Lakini akajibu, “Kwa nini kuniuliza Jina langu?” Ndipo akambariki huko.
30 Kwa hiyo Yakobo akapaita mahali pale Penieli‡maana yake Uso wa Mungu; sawa na Penueli kwa Kiebrania, akisema, “Ni kwa sababu nimemwona Mungu uso kwa uso, na bado uhai wangu umehifadhiwa.”
31 Jua lilikuwa linachomoza Yakobo alipoondoka Penueli, naye alikuwa akichechemea kwa sababu ya nyonga yake. 32 Kwa hiyo hadi leo Waisraeli hawali mshipa ulioungana na kiungio cha nyonga, kwa sababu kiungio cha nyonga ya Yakobo kiliteguliwa karibu na mshipa huo.