4
Pumziko aliloliahidi Mwenyezi Mungu
1 Kwa hiyo, kwa kuwa bado ahadi ya kuingia rahani iko wazi, tujihadhari ili hata mmoja wenu asije akaikosa. 2 Kwa maana sisi pia tumesikia Injili iliyohubiriwa kwetu, kama nao walivyosikia; lakini ujumbe ule waliousikia haukuwa na maana kwao, kwa sababu wale waliousikia hawakuuchanganya na imani. 3 Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha, kama vile Mungu alivyosema,
“Kwa hiyo nikaapa katika hasira yangu,
‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”
Lakini kazi yake ilikamilika tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 4 Kwa maana mahali fulani amezungumza kuhusu siku ya saba, akisema: “Katika siku ya saba Mungu alipumzika kutoka kazi zake zote.” 5 Tena hapo awali amesema, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”
6 Kwa hiyo inabaki kuwa wazi kwa wengine kuingia, nao wale wa kwanza waliopokea Injili walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii. 7 Kwa hiyo Mungu ameweka siku nyingine, akaiita “Leo”, akisema kwa kinywa cha Daudi baadaye sana, kwa maneno yaliyotangulia kunenwa:
“Leo, mkiisikia sauti yake,
msiifanye mioyo yenu migumu”.
8 Kwa maana kama Yoshua angelikuwa amewapa raha, Mungu hangesema tena baadaye kuhusu siku nyingine. 9 Basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu; 10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyopumzika kutoka kazi zake. 11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.
12 Kwa maana neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye lazima tutawajibika kwake.
Isa Al-Masihi ni Kuhani Mkuu kuliko wote
14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Isa Mwana wa Mungu*Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili., basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.