3
Isa ni mkuu kuliko Musa
Kwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Isa, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu. Alikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemteua, kama Musa alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu. Isa ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Musa, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe. Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu. Musa, kama mtumishi, alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale Mungu angeyasema baadaye. Lakini Al-Masihi ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.
Onyo dhidi ya kutokuamini
Kwa hiyo, kama Roho wa Mungu asemavyo:
“Leo, mkiisikia sauti yake,
msiifanye mioyo yenu migumu,
kama mlivyofanya katika uasi,
wakati ule wa kujaribiwa jangwani,
ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima,
ingawa kwa miaka arobaini
walikuwa wameyaona matendo yangu.
10 Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile,
nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka,
nao hawajazijua njia zangu.’
11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,
‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”
12 Ndugu zangu, chungeni asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai. 13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu inaitwa “Leo”, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. 14 Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Al-Masihi, tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho. 15 Kama ilivyonenwa:
“Leo, mkiisikia sauti yake,
msiifanye mioyo yenu migumu
kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”
16 Basi ni nani waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa? 17 Lakini ni nani Mungu aliwakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani? 18 Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii? 19 Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.