4
Shtaka dhidi ya Israeli 
  1 Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi Waisraeli,  
kwa sababu Mwenyezi Mungu analo shtaka  
dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi:  
“Hakuna uaminifu, hakuna upendo,  
hakuna kumjua Mungu katika nchi.   
 2 Kuna kulaani tu, uongo na uuaji,  
wizi na uzinzi,  
bila kuwa na mipaka,  
nao umwagaji damu mmoja  
baada ya mwingine.   
 3 Kwa sababu hii nchi huomboleza,  
wote wanaoishi ndani yake wanadhoofika;  
wanyama wa kondeni, ndege wa angani  
na samaki wa baharini wanakufa.   
 4 “Lakini mtu yeyote na asilete shtaka,  
mtu yeyote na asimlaumu mwenzake,  
kwa maana watu wako ni kama wale  
waletao mashtaka dhidi ya kuhani.   
 5 Unajikwaa usiku na mchana,  
nao manabii hujikwaa pamoja nawe.  
Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako:   
 6 watu wangu wanaangamizwa  
kwa kukosa maarifa.  
“Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa,  
mimi nami nitakukataa wewe  
usiwe kuhani kwangu mimi;  
kwa kuwa umeacha kuijali Torati ya Mungu wako  
mimi nami sitawajali watoto wako.   
 7 Kadiri makuhani walivyoongezeka,  
ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu,  
walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu.   
 8 Wanajilisha dhambi za watu wangu  
na kupendezwa na uovu wao.   
 9 Hata itakuwa: Kama walivyo watu,  
ndivyo walivyo makuhani.  
Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao  
na kuwalipa kwa matendo yao.   
 10 “Watakula lakini hawatashiba;  
watajiingiza katika ukahaba  
lakini hawataongezeka,  
kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu  
na kujiingiza wenyewe   
 11 katika ukahaba;  
kunywa divai ya zamani na divai mpya  
huondoa ufahamu   
 12 wa watu wangu.  
Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti  
nao hujibiwa na fimbo ya mti.  
Roho ya ukahaba imewapotosha,  
hawana uaminifu kwa Mungu wao.   
 13 Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima  
na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima,  
chini ya mialoni, milibua na miela,  
ambako kuna vivuli vizuri.  
Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba  
na wake za wana wenu uzinzi.   
 14 “Sitawaadhibu binti zenu wakati  
wanapogeukia ukahaba,  
wala wake za wana wenu  
wanapofanya uzinzi,  
kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya  
na kutambikia pamoja na makahaba  
wa mahali pa ibada za sanamu:  
watu wasiokuwa na ufahamu  
wataangamia!   
 15 “Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli,  
Yuda naye asije akawa na hatia.  
“Usiende Gilgali,  
usipande kwenda Beth-Aveni*maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu); yaani Betheli kwa dhihaka.  
Wala usiape,  
‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo!’   
 16 Waisraeli ni wakaidi,  
kama ndama jike mkaidi.  
Ni jinsi gani basi Mwenyezi Mungu anaweza kuwachunga  
kama wana-kondoo  
katika shamba la majani?   
 17 Efraimu amejiunga na sanamu,  
achana naye!   
 18 Hata wakati wamemaliza vileo vyao  
wanaendelea na ukahaba wao,  
watawala wao hupenda sana  
njia za aibu.   
 19 Kisulisuli kitawafagilia mbali  
na dhabihu zao zitawaletea aibu.