5
Hukumu dhidi ya Israeli
“Sikieni hili, enyi makuhani!
Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli!
Sikieni, ee nyumba ya mfalme!
Hukumu hii ni dhidi yenu:
Mmekuwa mtego huko Mispa,
wavu uliotandwa juu ya Tabori.
Waasi wamezidisha sana mauaji.
Mimi nitawatiisha wote.
Ninajua yote kuhusu Efraimu,
Israeli hukufichika kwangu.
Efraimu, sasa umegeukia ukahaba,
Israeli amenajisika.
 
“Matendo yao hayawaachii
kurudi kwa Mungu wao.
Roho ya ukahaba iko ndani ya mioyo yao,
hawamkubali Mwenyezi Mungu.
Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao;
Waisraeli, hata Efraimu,
wanajikwaa katika dhambi zao;
pia Yuda atajikwaa pamoja nao.
Wanapoenda na makundi yao ya kondoo na ng’ombe
kumtafuta Mwenyezi Mungu,
hawatampata;
yeye amejiondoa kutoka kwao.
Wao si waaminifu kwa Mwenyezi Mungu;
wamezaa watoto haramu.
Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi
zitawaangamiza wao
pamoja na mashamba yao.
 
“Pigeni tarumbeta huko Gibea,
na baragumu huko Rama.
Pazeni kelele za vita huko Beth-Aveni*maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu); yaani Betheli kwa dhihaka;
ongoza, ee Benyamini.
Efraimu ataachwa ukiwa
katika siku ya kuadhibiwa.
Miongoni mwa makabila ya Israeli
ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia.
10 Viongozi wa Yuda ni kama wale
wanaosogeza mawe ya mpaka.
Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao
kama mafuriko ya maji.
11 Efraimu amedhulumiwa,
amekanyagwa katika hukumu
kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu.
12 Mimi ni kama nondo kwa Efraimu,
na kama uozo kwa watu wa Yuda.
 
13 “Efraimu alipoona ugonjwa wake,
naye Yuda vidonda vyake,
ndipo Efraimu aligeukia Ashuru,
na kuomba msaada kwa mfalme mkuu.
Lakini hawezi kukuponya,
hawezi kukuponya vidonda vyako.
14 Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu,
kama simba mkubwa kwa Yuda.
Nitawararua vipande vipande na kuondoka;
nitawachukua mbali,
na hakuna wa kuwaokoa.
15 Kisha nitarudi mahali pangu
hadi watakapokubali kosa lao.
Nao watautafuta uso wangu;
katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”

*5:8 maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu); yaani Betheli kwa dhihaka