10
 1 Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana,  
alijizalia matunda mwenyewe.  
Kadiri matunda yake yalivyoongezeka,  
alijenga madhabahu zaidi;  
kadiri nchi yake ilivyostawi,  
alipamba mawe yake ya ibada.   
 2 Moyo wao ni mdanganyifu,  
nao sasa lazima wachukue hatia yao.  
Mwenyezi Mungu atabomoa madhabahu zao  
na kuharibu mawe yao ya ibada.   
 3 Kisha watasema, “Hatuna mfalme  
kwa sababu hatukumheshimu Mwenyezi Mungu.  
Lakini hata kama tungekuwa na mfalme,  
angeweza kutufanyia nini?”   
 4 Wanaweka ahadi nyingi,  
huapa viapo vya uongo  
wanapofanya mapatano;  
kwa hiyo mashtaka huchipuka  
kama magugu ya sumu  
katika shamba lililolimwa.   
 5 Watu wanaoishi Samaria huogopa  
kwa ajili ya sanamu ya ndama ya Beth-Aveni*maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu); yaani Betheli kwa dhihaka.  
Watu wake wataiombolezea,  
vivyo hivyo kuhani wake wa kuabudu sanamu,  
wale waliokuwa wamefurahia fahari yake,  
kwa sababu itaondolewa kutoka kwao  
kwenda uhamishoni.   
 6 Itachukuliwa kwenda Ashuru  
kama ushuru kwa mfalme mkuu.  
Efraimu atafedheheshwa;  
Israeli ataaibika kwa ajili ya sanamu zake za mti.   
 7 Samaria na mfalme wake wataelea  
kama kijiti juu ya maji.   
 8 Mahali pa juu pa uovu†yaani Aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni pataharibiwa:  
ndiyo dhambi ya Israeli.  
Miiba na mibaruti itaota  
na kufunika madhabahu zao.  
Kisha wataiambia milima, “Tufunikeni!”  
na vilima, “Tuangukieni!”   
 9 “Tangu siku za Gibea, umetenda dhambi, ee Israeli,  
huko ndiko ulibaki.  
Je, vita havikuwapata  
watenda maovu huko Gibea?   
 10 Wakati nitakapopenda, nitawaadhibu;  
mataifa yatakusanywa dhidi yao  
ili kuwaweka katika vifungo  
kwa ajili ya dhambi zao mbili.   
 11 Efraimu ni ndama jike aliyefundishwa  
ambaye hupenda kupura;  
hivyo nitamfunga nira  
juu ya shingo yake nzuri.  
Nitamwendesha Efraimu,  
Yuda lazima alime,  
naye Yakobo lazima avunjavunje  
mabonge ya udongo.   
 12 Jipandieni wenyewe haki,  
vuneni matunda ya upendo usio na kikomo,  
vunjeni ardhi yenu isiyolimwa;  
kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta Mwenyezi Mungu,  
hadi atakapokuja  
na kuwanyeshea juu yenu haki.   
 13 Lakini mmepanda uovu,  
mkavuna ubaya,  
mmekula tunda la udanganyifu.  
Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe  
na wingi wa mashujaa wenu,   
 14 mngurumo wa vita utainuka dhidi ya watu wako,  
na ngome zako zote zitaharibiwa:  
kama Shalmani alivyoharibu Beth-Arbeli katika siku ile ya vita,  
wakati mama pamoja na watoto wao  
walipotupwa kwa nguvu ardhini.   
 15 Ndivyo itakavyotokea kwako, ee Betheli,  
kwa sababu uovu wako ni mkuu.  
Siku ile itakapopambazuka,  
mfalme wa Israeli ataharibiwa kabisa.