9
Adhabu kwa Israeli 
  1 Usifurahie, ee Israeli;  
usishangilie kama mataifa mengine.  
Kwa kuwa hukuwa  
mwaminifu kwa Mungu wako;  
umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu  
ya kupuria nafaka.   
 2 Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai  
havitalisha watu,  
divai mpya itawapungukia.   
 3 Hawataishi katika nchi ya Mwenyezi Mungu,  
Efraimu atarudi Misri  
na atakula chakula  
kilicho najisi huko Ashuru.   
 4 Hawatammiminia Mwenyezi Mungu sadaka ya divai  
wala dhabihu zao hazitampendeza.  
Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao  
kama mkate wa waombolezaji;  
nao wote wazilao watakuwa najisi.  
Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe;  
kisije katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.   
 5 Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa,  
katika siku za sikukuu za Mwenyezi Mungu?   
 6 Hata ikiwa wataokoka maangamizi,  
Misri atawakusanya,  
nayo Memfisi*yaani Nofu itawazika.  
Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma,  
nayo miiba itafunika mahema yao.   
 7 Siku za adhabu zinakuja,  
siku za malipo zimewadia.  
Israeli na afahamu hili.  
Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana  
na uadui wenu ni mkubwa sana,  
nabii anadhaniwa ni mpumbavu,  
mtu aliyeongozwa na Mungu  
anaonekana mwendawazimu.   
 8 Nabii, pamoja na Mungu wangu,  
ndiye mlinzi juu ya Efraimu,  
hata hivyo mitego inamngojea  
katika mapito yake yote,  
na uadui katika nyumba ya Mungu wake.   
 9 Wamezama sana katika rushwa,  
kama katika siku za Gibea.  
Mungu atakumbuka uovu wao  
na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.   
 10 “Nilipompata Israeli, ilikuwa kama  
kupata zabibu jangwani;  
nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona  
matunda ya kwanza katika mtini.  
Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu  
kwa ile sanamu ya aibu,  
nao wakawa najisi  
kama kitu kile walichokipenda.   
 11 Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege:  
hakuna kuzaa, hakuna kubeba mimba,  
hakuna kuchukua mimba.   
 12 Hata wakilea watoto,  
nitamuua kila mmoja.  
Ole wao  
nitakapowapiga kisogo!   
 13 Nimemwona Efraimu, kama Tiro,  
aliyeoteshwa mahali pazuri.  
Lakini Efraimu wataleta  
watoto wao kwa mchinjaji.”   
 14 Wape, Ee Mwenyezi Mungu,  
je, utawapa nini?  
Wape tumbo zinazoharibu mimba  
na matiti yaliyokauka.   
 15 “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali,  
niliwachukia huko.  
Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi,  
nitawafukuza katika nyumba yangu.  
Sitawapenda tena,  
viongozi wao wote ni waasi.   
 16 Efraimu ameharibiwa,  
mzizi wao umenyauka,  
hawazai tunda.  
Hata kama watazaa watoto,  
nitawachinja wazao wao  
waliotunzwa vizuri.”   
 17 Mungu wangu atawakataa  
kwa sababu hawakumtii;  
watakuwa watu wa kutangatanga  
miongoni mwa mataifa.