8
Israeli kuvuna kisulisuli 
  1 “Wekeni tarumbeta midomoni mwenu!  
Tai yuko juu ya nyumba ya Mwenyezi Mungu  
kwa sababu watu wamevunja agano langu,  
wameasi dhidi ya sheria yangu.   
 2 Israeli ananililia,  
‘Ee Mungu wetu, tunakukubali!’   
 3 Lakini Israeli amekataa lile lililo jema,  
adui atamfuatia.   
 4 Wanaweka wafalme bila idhini yangu,  
wamechagua wakuu bila kibali changu.  
Kwa fedha zao na dhahabu  
wamejitengenezea sanamu kwa ajili  
ya maangamizi yao wenyewe.   
 5 Ee Samaria, tupilieni mbali sanamu yenu ya ndama!  
Hasira yangu inawaka dhidi yao.  
Watakuwa najisi hadi lini?   
 6 Zimetoka katika Israeli!  
Ndama huyu: ametengenezwa na fundi, si Mungu.  
Atavunjwa vipande vipande,  
yule ndama wa Samaria.   
 7 “Wanapanda upepo  
na kuvuna kisulisuli.  
Bua halina suke,  
halitatoa unga.  
Kama lingetoa nafaka,  
wageni wangeila yote.   
 8 Israeli amemezwa;  
sasa yupo miongoni mwa mataifa  
kama kitu kisicho na thamani.   
 9 Kwa kuwa wamepanda kwenda Ashuru  
kama punda-mwitu anayetangatanga peke yake.  
Efraimu amejiuza mwenyewe  
kwa wapenzi.   
 10 Ingawa wamejiuza wenyewe miongoni mwa mataifa,  
sasa nitawakusanya pamoja.  
Wataanza kudhoofika chini ya uonevu  
wa mfalme mwenye nguvu.   
 11 “Ingawa Efraimu alijenga madhabahu nyingi  
kwa ajili ya sadaka za dhambi,  
hizi zimekuwa madhabahu  
za kufanyia dhambi.   
 12 Niliwaandikia mambo mengi yaliyohusu sheria yangu,  
lakini waliziangalia kama kitu kigeni.   
 13 Wanatoa dhabihu nilizopewa mimi  
nao wanakula hiyo nyama,  
lakini Mwenyezi Mungu hapendezwi nao.  
Sasa ataukumbuka uovu wao  
na kuadhibu dhambi zao:  
Watarudi Misri.   
 14 Israeli amemsahau Muumba wake  
na kujenga majumba ya kifalme,  
Yuda amejengea miji mingi ngome.  
Lakini nitatuma moto kwenye miji yao  
utakaoteketeza ngome zao.”