7
 1 kila mara nilipotaka kumponya Israeli,  
dhambi za Efraimu zinafichuliwa  
na maovu ya Samaria yanafunuliwa.  
Wanafanya udanganyifu,  
wezi huvunja nyumba,  
maharamia hunyang’anya barabarani,   
 2 lakini hawafahamu kwamba  
ninakumbuka matendo yao yote mabaya.  
Dhambi zao zimewameza,  
ziko mbele zangu siku zote.   
 3 “Wanamfurahisha sana mfalme kwa maovu yao,  
wakuu wao kwa uongo wao.   
 4 Wote ni wazinzi,  
wanawaka kama tanuru  
ambalo moto wake mwokaji hana haja ya kuuchochea  
kuanzia kukanda unga  
hadi umekwisha kuumuka.   
 5 Katika sikukuu ya mfalme wetu  
wakuu wanawaka kwa mvinyo,  
naye anawaunga mkono wenye mizaha.   
 6 Mioyo yao ni kama tanuru,  
wanamwendea kwa hila.  
Hasira yao inafoka moshi usiku kucha,  
wakati wa asubuhi inalipuka  
kama miali ya moto.   
 7 Wote ni moto kama tanuru;  
wanawaangamiza watawala wao.  
Wafalme wake wote wanaanguka,  
wala hakuna yeyote kati yao aniitaye mimi.   
 8 “Efraimu anajichanganya na mataifa;  
Efraimu ni mkate ambao haukuiva.   
 9 Wageni wananyonya nguvu zake,  
lakini hafahamu hilo.  
Nywele zake zina mvi hapa na pale,  
lakini hana habari.   
 10 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yake,  
lakini pamoja na haya yote  
harudi kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake,  
wala kumtafuta.   
 11 “Efraimu ni kama hua,  
hudanganywa kwa urahisi na hana akili:  
mara anaita Misri,  
mara anageukia Ashuru.   
 12 Watakapoenda, nitatupa wavu wangu juu yao;  
nitawavuta chini waanguke kama ndege wa angani.  
Nitakaposikia wakikusanyika pamoja,  
nitawanasa.   
 13 Ole wao, kwa sababu  
wamepotoka kutoka kwangu!  
Maangamizi ni yao  
kwa sababu wameniasi!  
Ninatamani kuwakomboa,  
lakini wanasema uongo dhidi yangu.   
 14 Hawanililii mimi kutoka mioyoni mwao,  
bali wanaomboleza vitandani mwao.  
Hukusanyika pamoja kwa ajili ya nafaka na divai mpya,  
lakini hugeukia mbali nami.   
 15 Niliwafundisha na kuwatia nguvu,  
lakini wanapanga mabaya dhidi yangu.   
 16 Hawamgeukii Yeye Aliye Juu Sana,  
wako kama upinde wenye kasoro.  
Viongozi wao wataanguka kwa upanga  
kwa sababu ya maneno yao ya jeuri.  
Kwa ajili ya hili watadhihakiwa  
katika nchi ya Misri.