14
Toba iletayo baraka 
  1 Rudi, ee Israeli, kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako.  
Dhambi zako zimekuwa anguko lako!   
 2 Chukueni maneno pamoja nanyi,  
mkamrudie Mwenyezi Mungu.  
Mwambieni:  
“Samehe dhambi zetu zote  
na utupokee kwa neema,  
ili tuweze kutoa matunda yetu  
kama sadaka za mafahali.   
 3 Ashuru hawezi kutuokoa,  
hatutapanda farasi wa vita.  
Kamwe hatutasema tena ‘miungu yetu’  
kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza,  
kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”   
 4 “Nitaponya ukaidi wao  
na kuwapenda kwa hiari yangu,  
kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.   
 5 Nitakuwa kama umande kwa Israeli;  
atachanua kama yungiyungi.  
Kama mwerezi wa Lebanoni  
atashusha mizizi yake chini;   
 6 matawi yake yatatanda.  
Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni,  
harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.   
 7 Watu wataishi tena kwenye kivuli chake.  
Atastawi kama nafaka.  
Atachanua kama mzabibu,  
nao umaarufu wake utakuwa  
kama divai inayotoka Lebanoni.   
 8 Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu?  
Nitamjibu na kumtunza.  
Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi;  
kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”   
 9 Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya.  
Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa.  
Njia za Mwenyezi Mungu ni adili;  
wenye haki huenda katika njia hizo,  
lakini waasi watajikwaa ndani yake.