Yoeli
1
Neno la Mwenyezi Mungu ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli.
 
Kuvamiwa wa nzige
Sikilizeni hili, enyi wazee;
sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi.
Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea
katika siku zenu au katika siku za babu zenu?
Waelezeni watoto wenu,
na watoto wenu wawaambie watoto wao,
na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.
Kilichosazwa na kundi la tunutu
nzige wakubwa wamekula,
kilichosazwa na nzige wakubwa
parare wamekula,
kilichosazwa na parare
madumadu wamekula.
 
Amkeni, enyi walevi, mlie!
Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo,
pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya,
kwa kuwa mmenyang’anywa
kutoka midomoni mwenu.
Taifa limevamia nchi yangu,
lenye nguvu tena lisilo na idadi;
lina meno ya simba,
magego ya simba jike.
Limeharibu mizabibu yangu
na kuangamiza mitini yangu.
Limebambua magome yake
na kuyatupilia mbali,
likayaacha matawi yake yakiwa meupe.
 
Omboleza kama bikira aliyevaa gunia
akimwomboleza mume wa ujana wake.
Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji
zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Mwenyezi Mungu.
Makuhani wanaomboleza,
wale wanaohudumu mbele za Mwenyezi Mungu.
10 Mashamba yameharibiwa,
ardhi imekauka;
nafaka imeharibiwa,
mvinyo mpya umekauka,
mafuta yamekoma.
 
11 Kateni tamaa, enyi wakulima,
lieni, enyi mlimao mizabibu;
huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri,
kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa.
12 Mzabibu umekauka
na mtini umenyauka;
mkomamanga, mtende na mtofaa,
miti yote shambani, imekauka.
Hakika furaha yote ya mwanadamu
imeondoka.
Wito wa kuomboleza
13 Vaeni gunia, enyi makuhani, mwomboleze;
pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni.
Njooni, vaeni gunia usiku kucha,
enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu;
kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji
zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.
14 Tangazeni saumu takatifu;
liiteni kusanyiko takatifu.
Waiteni wazee
na wote wanaoishi katika nchi
waende katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,
wakamlilie Mwenyezi Mungu.
 
15 Ole kwa siku hiyo!
Kwa kuwa siku ya Mwenyezi Mungu iko karibu;
itakuja kama uharibifu
kutoka kwa Mwenyezi.*Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.
 
16 Je, chakula hakikukatiliwa mbali
mbele ya macho yetu:
furaha na shangwe
kutoka nyumba ya Mungu wetu?
17 Mbegu zinakauka
chini ya mabonge ya udongo.
Maghala yameachwa katika uharibifu,
maghala ya nafaka yamebomolewa,
kwa maana hakuna nafaka.
18 Jinsi gani ng’ombe wanavyolia!
Makundi ya mifugo yanahangaika
kwa sababu hawana malisho;
hata makundi ya kondoo yanateseka.
 
19 Kwako, Ee Mwenyezi Mungu, naita,
kwa kuwa moto umeteketeza
malisho ya mbugani
na miali ya moto imeunguza
miti yote shambani.
20 Hata wanyama pori wanakuonea shauku;
vijito vya maji vimekauka,
na moto umeteketeza
malisho yote ya mbugani.

*1:15 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.