Isaya
1
1 Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.
Taifa asi
2 Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia!
Kwa maana Mwenyezi Mungu amesema:
“Nimewalisha watoto na kuwalea,
lakini wameniasi mimi.
3 Ng’ombe anamjua bwana wake,
naye punda anajua hori la mmiliki wake,
lakini Israeli hajui,
watu wangu hawaelewi.”
4 Ole wa taifa lenye dhambi,
watu waliolemewa na uovu,
uzao wa watenda mabaya,
watoto waliozoelea upotovu!
Wamemwacha Mwenyezi Mungu,
Wamemkataa kwa dharau
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli
na kumgeuzia kisogo.
5 Kwa nini mzidi kupigwa?
Kwa nini kudumu katika uasi?
Kichwa chako chote kimejeruhiwa,
moyo wako wote ni mgonjwa.
6 Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako
hakuna uzima:
ni majeraha matupu na makovu
na vidonda vinavyotoa damu,
havikusafishwa au kufungwa
wala kulainishwa kwa mafuta.
7 Nchi yenu imekuwa ukiwa,
miji yenu imeteketezwa kwa moto;
mashamba yenu yameachwa tupu na wageni
mbele ya macho yenu,
yameharibiwa kama yaliyopinduliwa na wageni.
8 Binti Sayuni ameachwa kama kipenu
katika shamba la mizabibu,
kama kibanda katika shamba la matango,
kama mji uliozingirwa.
9 Kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni*Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni hapa ni Yahweh Sabaoth; pia Warumi 9:29 na Yakobo 5:4.
hakutuachia walionusurika,
tungekuwa kama Sodoma,
tungefanana na Gomora.
10 Sikieni neno la Mwenyezi Mungu,
ninyi watawala wa Sodoma;
sikilizeni Torati ya Mungu wetu,
enyi watu wa Gomora!
11 Mwenyezi Mungu anasema, “Wingi wa sadaka zenu,
ni kitu gani kwangu?
Nina sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi,
za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona.
Sipendezwi na damu za mafahali
wala za wana-kondoo na mbuzi.
12 Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu,
ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo,
huku kuzikanyaga nyua zangu?
13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!
Uvumba wenu ni chukizo kwangu.
Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.
14 Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi,
na sikukuu zenu zilizoamriwa:
moyo wangu unazichukia kabisa.
Zimekuwa mzigo kwangu,
nimechoka kuzivumilia.
15 Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi,
nitaficha macho yangu nisiwaone;
hata mkiomba maombi mengi
sitasikiliza.
“Mikono yenu imejaa damu!
16 “Jiosheni na mkajitakase.
Yaondoeni matendo yenu maovu mbele zangu;
acheni kutenda mabaya.
17 Jifunzeni kutenda mema, tafuteni haki.
Wateteeni waliodhulumiwa.
Teteeni shauri la yatima,
wateteeni wajane.
18 “Njooni basi tujadiliane,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,
zitakuwa nyeupe kama theluji;
ingawa ni nyekundu sana kama damu,
zitakuwa nyeupe kama sufu.
19 Mkikubali na kutii,
mtakula mema ya nchi,
20 lakini mkikataa na kuasi,
mtaangamizwa kwa upanga.”
Kwa kuwa kinywa cha Mwenyezi Mungu kimenena.
21 Tazama jinsi mji uliokuwa mwaminifu
umekuwa kahaba!
Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu,
haki ilikuwa inakaa ndani yake,
lakini sasa ni wauaji!
22 Fedha yenu imekuwa takataka,
divai yenu nzuri imechanganywa na maji.
23 Watawala wenu ni waasi,
rafiki wa wezi,
wote wanapenda rushwa
na kukimbilia hongo.
Hawatetei yatima;
shauri la mjane haliletwi mbele yao.
24 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi:
“Lo! Nitapata faraja kutoka kwa adui zangu,
na kujilipizia kisasi kwa watesi wangu.
25 Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu,
nitawasafisha takataka zenu zote
na kuwaondolea unajisi wenu wote.
26 Nitawarudishia waamuzi wenu kama ilivyokuwa siku za zamani,
nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni.
Baadaye utaitwa,
Mji wa Haki,
Mji Mwaminifu.”
27 Sayuni itakombolewa kwa haki,
wale walio ndani yake waliotubu, kwa uaminifu.
28 Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa,
nao wanaomwacha Mwenyezi Mungu wataangamia.
29 “Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni
ambayo mlifurahia,
mtafadhaika kwa sababu ya bustani
mlizozichagua.
30 Mtakuwa kama mwaloni ulio na majani yanayonyauka,
kama bustani isiyokuwa na maji.
31 Mtu mwenye nguvu atatoweka kama majani makavu yanayowaka moto,
na kazi yake kama cheche ya moto;
vyote vitaungua pamoja,
wala hakuna wa kuuzima huo moto.”
*1:9 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni hapa ni Yahweh Sabaoth; pia Warumi 9:29 na Yakobo 5:4.