7
Ishara ya Imanueli
Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramu*yaani Shamu, na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda.
Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo mioyo ya Ahazi na watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo.
Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubumaana yake Mabaki Watarudi, mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi. Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia. Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga njama ili wakuangamize, wakisema, “Tuishambulie Yuda, naam, tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu, na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.” Lakini Bwana Mungu Mwenyezi asema hivi:
“ ‘Jambo hili halitatendeka,
halitatukia,
kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski,
na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake.
Katika muda wa miaka sitini na tano,
Efraimu atakuwa ameharibiwa
kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa.
Kichwa cha Efraimu ni Samaria,
na kichwa cha Samaria
ni mwana wa Remalia peke yake.
Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu,
hamtaimarika kamwe.’ ”
10 Mwenyezi Mungu akasema na Ahazi tena, 11 “Mwombe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ishara, iwe kwenye vina virefu sana, au kwenye vimo virefu sana.”
12 Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribu Mwenyezi Mungu.”
13 Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia? 14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanuelimaana yake Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. 15 Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema. 16 Lakini kabla mtoto hajajua kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa. 17 Mwenyezi Mungu ataleta juu yako pamoja na watu wako na juu ya nyumba ya baba yako, nyakati ambazo hazijawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda: naye Mwenyezi Mungu atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”
18 Katika siku ile Mwenyezi Mungu atawapigia filimbi inzi kutoka vijito vya mbali vya Misri, na nyuki kutoka nchi ya Ashuru. 19 Wote watakuja na kukaa kwenye mabonde yenye miteremko, na kwenye nyufa za miamba, kwenye vichaka vyote vyenye miiba, na kwenye mashimo yote ya maji. 20 Katika siku ile Bwana atatumia wembe ulioajiriwa kutoka ng’ambo ya Mto§yaani Mto Frati, yaani mfalme wa Ashuru, kunyoa nywele za kichwa chako na malaika ya miguu yako, na kuziondoa ndevu zako pia. 21 Katika siku ile, mtu atahifadhi hai mtamba mmoja na kondoo wawili. 22 Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali. 23 Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli elfu moja*Shekeli 1,000 ni kama kilo 11.5. za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu. 24 Watu wataenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba. 25 Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtaenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba. Patakuwa mahali ng’ombe wataachiwa huru, na kondoo kukimbia kimbia.

*7:1 yaani Shamu

7:3 maana yake Mabaki Watarudi

7:14 maana yake Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi

§7:20 yaani Mto Frati

*7:23 Shekeli 1,000 ni kama kilo 11.5.