8
Isaya na wanawe kama ishara
Mwenyezi Mungu akaniambia, “Chukua kitabu kikubwa, uandike kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi*maana yake Haraka kuteka nyara, upesi kwenye hizo nyara. Nami nitawaita kuhani Uria, na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.”
Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi. Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”
Mwenyezi Mungu akasema nami tena:
“Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yanayotiririka taratibu
wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia;
kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao
mafuriko makubwa ya Mtoyaani Mto Frati:
yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote.
Yatafurika juu ya mifereji yake yote,
yatamwagikia juu ya kingo zake zote,
na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake,
yakipita katikati na yakifika hadi shingoni.
Mabawa yake yaliyokunjuliwa
yatafunika upana wa nchi yako,
Ee Imanuelimaana yake Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi!”
 
Inueni ukelele wa vita, enyi mataifa,
na mkavunjwevunjwe!
Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali.
Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!
Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!
10 Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa;
fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa,
kwa maana Mungu yu pamoja nasi§Kiebrania ni Imanueli.
11 Mwenyezi Mungu alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:
12 “Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina,
usiogope kile wanachokiogopa,
wala usikihofu.
13 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndiye peke yake
ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu,
ndiye peke yake utakayemwogopa,
ndiye peke yake utakayemhofu,
14 naye atakuwa mahali patakatifu;
lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa
jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa
na mwamba wa kuwaangusha.
Kwa watu wa Yerusalemu,
atakuwa mtego na tanzi.
15 Wengi wao watajikwaa;
wataanguka na kuvunjika,
watategwa na kunaswa.”
 
16 Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria
miongoni mwa wanafunzi wangu.
17 Nitamngojea Mwenyezi Mungu,
ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake.
Nitaliweka tumaini langu kwake.
18 Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mwenyezi Mungu amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.
19 Watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunong’ona na kunung’unika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai? 20 Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko. 21 Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao. 22 Kisha wataangalia duniani na kuona tu dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.

*8:1 maana yake Haraka kuteka nyara, upesi kwenye hizo nyara

8:7 yaani Mto Frati

8:8 maana yake Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi

§8:10 Kiebrania ni Imanueli