20
Unabii dhidi ya Misri na Kushi
Mwaka ule jemadari mkuu alitumwa na Mfalme Sargoni wa Ashuru, naye akaja Ashdodi, akaushambulia na kuuteka, wakati huo Mwenyezi Mungu alisema kwa kinywa cha Isaya mwana wa Amozi. Akamwambia, “Vua gunia kutoka mwilini mwako na viatu kutoka miguuni mwako.” Naye akafanya hivyo, akitembea uchi, bila viatu.
Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Kama mtumishi wangu Isaya alivyotembea uchi na bila viatu kwa miaka mitatu, kama ishara na dalili mbaya dhidi ya nchi ya Misri na Kushi, vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawaongoza mateka wa Wamisri, na watu wa uhamisho wa Kushi, uchi na bila viatu, vijana hata wazee, wakiwa matako wazi, kwa aibu ya Wamisri. Wale waliotegemea Kushi na kujivunia Misri wataogopa na kuaibika. Katika siku ile watu wanaoishi katika pwani hii watasema, ‘Tazama lililowapata wale tuliowategemea, wale tuliowakimbilia kwa msaada na wokovu kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru! Tutawezaje basi kupona?’ ”