21
Unabii dhidi ya Babeli
Neno la unabii kuhusu Jangwa kando ya Bahari:
Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini,
mshambuliaji anakuja kutoka jangwani,
kutoka nchi inayotisha.
 
Nimeoneshwa maono ya kutisha:
Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara.
Elamu, shambulia! Umedi, zingira kwa jeshi!
Nitakomesha huzuni zote alizosababisha.
 
Kwa sababu hii, mwili wangu umeteswa na maumivu,
maumivu makali ya ghafula yamenishika,
kama yale ya mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa.
Nimeduwazwa na lile ninalolisikia,
nimeshangazwa na lile ninaloliona.
Moyo wangu unababaika,
woga unanifanya nitetemeke,
gizagiza la jioni nililolitamani sana,
limekuwa hofu kuu kwangu.
 
Wanaandaa meza,
wanatandaza mazulia,
wanakula, wanakunywa!
Amkeni, enyi maafisa,
zitieni ngao mafuta!
Hili ndilo Bwana analoniambia:
“Nenda, weka mlinzi,
na atoe taarifa ya kile anachokiona.
Anapoona magari ya vita
pamoja na kundi la farasi,
wapanda punda au wapanda ngamia,
na awe macho, awe macho kikamilifu.”
Naye mlinzi alipaza sauti,
“Mchana baada ya mchana, bwana wangu,
ninasimama katika mnara wa ulinzi,
kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa.
Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita
pamoja na kundi la farasi.
Naye anajibu:
‘Babeli umeanguka, umeanguka!
Vinyago vyote vya miungu yake
vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ”
 
10 Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria,
ninawaambia kile nilichokisikia
kutoka kwa Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
kutoka kwa Mungu wa Israeli.
Unabii dhidi ya Edomu
11 Neno la unabii kuhusu Duma:
Mtu fulani ananiita kutoka Seiri,
“Mlinzi, usiku utaisha lini?
Mlinzi, usiku utaisha lini?”
12 Mlinzi anajibu,
“Asubuhi inakuja, lakini pia usiku.
Ukitaka kuuliza, basi uliza;
na urudi mara tena.”
Unabii dhidi ya Arabia
13 Neno la unabii kuhusu Arabia:
Enyi misafara ya Wadedani,
mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia,
14 leteni maji kwa wenye kiu,
ninyi mnaoishi Tema,
leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi.
15 Wanaukimbia upanga,
upanga uliochomolewa alani,
kutoka upinde uliopindwa,
na kutoka kwa joto la vita.
16 Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho. 17 Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.” Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, amesema.