22
Unabii kuhusu Yerusalemu
1 Neno la unabii kuhusu Bonde la Maono:
Nini kinachokutaabisha sasa,
kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?
2 Ewe mji uliojaa ghasia,
ewe mji wa makelele na sherehe!
Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga,
wala hawakufa vitani.
3 Viongozi wako wote wamekimbia pamoja,
wamekamatwa bila kutumia upinde.
Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja,
mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.
4 Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami,
niache nilie kwa uchungu.
Usijaribu kunifariji
juu ya maangamizi ya watu wangu.”
5 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, anayo siku
ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya
katika Bonde la Maono,
siku ya kuangusha kuta
na ya kupiga kelele hadi milimani.
6 Elamu analichukua podo,
pamoja na waendesha magari ya vita na farasi.
Kiri anaifungua ngao.
7 Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita,
nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji.
8 Ulinzi wa Yuda umeondolewa.
Nawe ulitazama siku ile
silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni.
9 Mkaona kuwa Mji wa Daudi
una matundu mengi katika ulinzi wake,
mkaweka akiba ya maji
kwenye Bwawa la Chini.
10 Mlihesabu majengo katika Yerusalemu
nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.
11 Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili
kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani,
lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza,
au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale.
12 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
aliwaita siku ile
ili kulia na kuomboleza,
kung’oa nywele zenu na kuvaa magunia.
13 Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,
kuchinja ng’ombe na kuchinja kondoo,
kula nyama na kunywa mvinyo!
Mnasema, “Tuleni na kunywa,
kwa kuwa kesho tutakufa!”
14 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amelifunua hili nikiwa ninasikia: Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema: “Hadi siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”
15 Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asemalo:
“Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna,
ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme:
16 Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa
kujikatia kaburi lako mwenyewe,
ukichonga kaburi lako mahali palipo juu,
na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba?
17 “Jihadhari, Mwenyezi Mungu yu karibu kukukamata thabiti,
na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu.
18 Atakuvingirisha uwe kama mpira
na kukutupa katika nchi kubwa.
Huko ndiko utakakofia,
na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia,
na kuwa fedheha kwa nyumba ya bwana wako!
19 Nitakuondoa kutoka kazi yako,
nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako.
20 “Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia. 21 Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda. 22 Nitaweka begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua. 23 Nitampigilia kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake. 24 Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Wazao wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”
25 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni asema, “Katika siku ile, kigingi kilichopigiliwa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioning’inia juu yake utaanguka chini.” Mwenyezi Mungu amesema.