23
Unabii kuhusu Tiro
1 Neno la unabii kuhusu Tiro:
Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi!
Kwa kuwa Tiro imeangamizwa,
imeachwa bila nyumba wala bandari.
Kuanzia nchi ya Kitimu*yaani Kipro, kisiwa katika Bahari ya Mediterania
neno limewajia.
2 Nyamazeni kimya, enyi watu wa kisiwani,
pia ninyi wafanyabiashara wa Sidoni,
ambao mabaharia wamewatajirisha.
3 Kwenye maji makuu
nafaka za Shihori zilikuja;
mavuno ya Mto Naili yalikuwa mapato ya Tiro,
naye akawa soko la mataifa.
4 Uaibishwe ee Sidoni, nawe ee ngome la bahari,
kwa kuwa bahari imesema:
“Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa wala sijapata kuzaa,
wala sijapata kulea wana wala kutunza binti.”
5 Habari ifikapo Misri,
watakuwa katika maumivu makuu kwa ajili ya taarifa kutoka Tiro.
6 Vukeni hadi Tarshishi,
ombolezeni, enyi watu wa kisiwani.
7 Je, huu ndio mji wenu uliojaa sherehe,
mji wa zamani, zamani kabisa
ambao miguu yake imeuchukua
kufanya makao nchi za mbali sana?
8 Ni nani amepanga hili dhidi ya Tiro,
mji utoao mataji,
ambao wafanyabiashara wake ni wana wa mfalme
na wachuuzi wake ni watu mashuhuri wa dunia?
9 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndiye alipanga jambo hili,
ili kukishusha kiburi cha utukufu wote
na kuwanyenyekeza wale wote
ambao ni mashuhuri duniani.
10 Ee Binti Tarshishi,
pita katika nchi yako kama vile Mto Naili
kwa kuwa huna tena bandari.
11 Mwenyezi Mungu amenyoosha mkono wake juu ya bahari
na kuzifanya falme zake zitetemeke.
Ametoa amri kuhusu Kanaani
kwamba ngome zake ziangamizwe.
12 Alisema, “Usizidi kufurahi,
ee Bikira Binti Sidoni, sasa umepondwa!
“Simama, vuka uende Kitimu;
hata huko hutapata pumziko.”
13 Tazama katika nchi ya Wakaldayo,
watu hawa ambao sasa hawaonekani kama wapo!
Waashuru wameifanya nchi hiyo
kuwa mahali pa viumbe wa jangwani.
Wamesimamisha minara yao ya kuuzingira,
wameziteka ngome zake na kuziacha tupu
na kuufanya kuwa magofu.
14 Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi;
ngome yenu imeangamizwa!
15 Wakati huo Tiro utasahauliwa kwa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Lakini mwisho wa miaka hiyo sabini, itakuwa kwa Tiro kama ilivyo katika wimbo wa kahaba:
16 “Twaa kinubi, tembea mjini kote,
ewe kahaba uliyesahauliwa;
piga kinubi vizuri, imba nyimbo nyingi,
ili upate kukumbukwa.”
17 Mwishoni mwa miaka sabini, Mwenyezi Mungu atatembelea Tiro. Naye Tiro atarudia ajira yake ya ukahaba, na atafanya biashara yake na falme zote duniani. 18 Lakini faida na mapato yake yatawekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu; hayatahifadhiwa wala kufichwa. Faida zake zitaenda kwa wale wanaoishi mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya chakula tele na mavazi mazuri.