24
Dunia kuharibiwa
Tazama, Mwenyezi Mungu ataifanya dunia kuwa ukiwa
na kuiharibu,
naye atauharibu uso wake
na kutawanya wanaoishi ndani yake:
ndivyo itakavyokuwa
kwa makuhani na kwa watu,
kwa bwana na kwa mtumishi,
kwa bibi na kwa mjakazi wake,
kwa muuzaji na kwa mnunuzi,
kwa mkopaji na kwa mkopeshaji,
kwa mdaiwa na kwa mdai.
Dunia itaharibiwa kabisa
na kutekwa nyara kabisa.
Mwenyezi Mungu amesema neno hili.
 
Dunia inakauka na kunyauka,
dunia inanyong’onyea na kunyauka,
waliotukuzwa wa dunia wananyong’onyea.
Dunia imetiwa unajisi na watu wake;
wameacha kutii sheria,
wamevunja amri
na kuvunja agano la milele.
Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia,
watu wake lazima waichukue hatia yao.
Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa,
nao waliosalia ni wachache sana.
Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka,
watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni.
Furaha ya matoazi imekoma,
kelele za wenye furaha zimekoma,
shangwe za kinubi zimenyamaza.
Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo,
kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.
10 Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa,
mlango wa kila nyumba umefungwa.
11 Barabarani wanalilia kupata mvinyo,
furaha yote imegeuka kuwa majonzi,
furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.
12 Mji umeachwa katika uharibifu,
lango lake limevunjwa vipande.
13 Ndivyo itakavyokuwa duniani
na miongoni mwa mataifa,
kama vile wakati mzeituni upigwavyo,
au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa.
 
14 Wanapaza sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha,
kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Mwenyezi Mungu.
15 Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni Mwenyezi Mungu utukufu,
liadhimisheni jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli,
katika visiwa vya bahari.
16 Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji:
“Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.”
 
Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika!
Ole wangu!
Watenda hila wanasaliti!
Kwa hila watenda hila wanasaliti!”
17 Hofu, shimo na mtego vinakungojea,
ewe mtu ukaaye duniani.
18 Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu
atatumbukia shimoni,
naye yeyote apandaye kutoka shimoni,
atanaswa kwenye mtego.
 
Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa,
misingi ya dunia inatikisika.
19 Dunia imepasuka,
dunia imechanika,
dunia imetikiswa kabisa.
20 Dunia inapepesuka kama mlevi,
inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo;
imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake
na ikianguka kamwe haitainuka tena.
 
21 Katika siku ile Mwenyezi Mungu ataadhibu
mamlaka zilizo juu mbinguni,
na wafalme walio chini duniani.
22 Watakusanywa pamoja
kama wafungwa waliofungwa gerezani;
watafungiwa gerezani
na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.
23 Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa;
kwa maana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni atatawala
juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu,
tena mbele ya wazee wake, kwa utukufu.