50
Dhambi ya Israeli na utii wa mtumishi
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Iko wapi hati ya talaka ya mama yako
ambayo kwayo niliachana naye?
Au nimewauza ninyi kwa nani
miongoni mwa watu wanaonidai?
Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa,
kwa sababu ya makosa, mama yenu aliachwa.
Nilipokuja, kwa nini hapakuwa hata mtu mmoja?
Nilipoita, kwa nini hapakuwa hata mtu mmoja wa kujibu?
Je, mkono wangu ni mfupi mno hata nisiweze kuwakomboa?
Je, mimi sina nguvu za kukuokoa?
Kwa kukemea tu naikausha bahari,
naigeuza mito ya maji kuwa jangwa;
samaki wake wanaoza kwa kukosa maji
na kufa kwa ajili ya kiu.
Ninalivika anga weusi na kufanya gunia
kuwa kifuniko chake.”
 
Bwana Mungu Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa,
ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka.
Huniamsha asubuhi kwa asubuhi,
huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye.
Bwana Mungu Mwenyezi amezibua masikio yangu,
nami sikuwa mwasi,
wala sikurudi nyuma.
Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao,
mashavu yangu wale wang’oao ndevu zangu;
sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha
na kutemewa mate.
Kwa sababu Bwana Mungu Mwenyezi ananisaidia,
sitatahayarika.
Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume,
nami ninajua sitaaibika.
Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu.
Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu?
Tukabiliane uso kwa uso!
Mshtaki wangu ni nani?
Ni nani aliye mshtaki wangu?
Ni Bwana Mungu Mwenyezi anisaidiaye mimi.
Ni nani huyo atakayenihukumu?
Wote watachakaa kama vazi,
nondo watawala wawamalize.
 
10 Ni nani miongoni mwenu amchaye Mwenyezi Mungu,
na kulitii neno la mtumishi wake?
Yeye atembeaye gizani,
yeye asiye na nuru,
na alitumainie jina la Mwenyezi Mungu,
na amtegemee Mungu wake.
11 Lakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto,
na kupeana mienge iwakayo ninyi kwa ninyi,
nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu
na ya mienge mliyoiwasha.
Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu:
Mtalala chini kwa mateso makali.