51
Wokovu wa milele kwa Sayuni
“Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki
na mnaomtafuta Mwenyezi Mungu:
Tazameni mwamba ambako mlichongwa,
na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;
mwangalieni Ibrahimu, baba yenu,
na Sara, ambaye aliwazaa.
Wakati nilimwita alikuwa mmoja tu,
nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.
Hakika Mwenyezi Mungu ataifariji Sayuni,
naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote;
atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni,
nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya Mwenyezi Mungu.
Shangwe na furaha zitakuwa ndani yake,
shukrani na sauti za kuimba.
 
“Nisikilizeni, watu wangu;
nisikieni, taifa langu:
Torati itatoka kwangu;
haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.
Haki yangu inakaribia mbio,
wokovu wangu unakuja,
nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.
Visiwa vitanitegemea
na kungojea mkono wangu kwa matumaini.
Inueni macho yenu mbinguni,
mkaitazame dunia chini;
mbingu zitatoweka kama moshi,
dunia itachakaa kama vazi,
na wakazi wake kufa kama inzi.
Bali wokovu wangu utadumu milele,
haki yangu haitakoma kamwe.
 
“Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa,
ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu:
Msiogope mashutumu ya wanadamu
wala msitiwe hofu na matukano yao.
Kwa maana nondo atawala kama vazi,
nao funza atawatafuna kama sufu.
Lakini haki yangu itadumu milele,
wokovu wangu kwa vizazi vyote.”
 
Amka, Amka! Jivike nguvu,
ewe mkono wa Mwenyezi Mungu,
Amka, kama siku zilizopita,
kama vile vizazi vya zamani.
Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande,
uliyemchoma huyo mnyama mkubwa?
10 Si ni wewe uliyekausha bahari,
maji ya kilindi kikuu,
uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari
ili waliokombolewa wapate kuvuka?
11 Wale waliolipiwa fidia na Mwenyezi Mungu watarudi.
Wataingia Sayuni wakiimba;
furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao.
Furaha na shangwe zitawapata,
huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.
 
12 “Mimi, naam mimi,
ndimi niwafarijie ninyi.
Ninyi ni nani hata kuwaogopa
wanadamu wanaokufa,
wanadamu ambao ni majani tu,
13 kwamba mnamsahau Mwenyezi Mungu Muumba wenu,
aliyezitanda mbingu
na kuiweka misingi ya dunia,
kwamba mnaishi katika hofu siku zote
kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu,
ambaye nia yake ni kuangamiza?
Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu?
14 Wafungwa waliojikunyata kwa hofu
watawekwa huru karibuni;
hawatafia kwenye gereza lao,
wala hawatakosa chakula.
15 Kwa maana Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako,
ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume:
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.
16 Nimeweka maneno yangu kinywani mwako
na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu:
Mimi niliyeweka mbingu mahali pake,
niliyeweka misingi ya dunia,
niwaambiaye Sayuni,
‘Ninyi ni watu wangu.’ ”
Kikombe cha ghadhabu ya Mwenyezi Mungu
17 Amka, amka!
Simama, ee Yerusalemu,
wewe uliyekunywa kutoka mkono wa Mwenyezi Mungu
kikombe cha ghadhabu yake,
wewe uliyekunywa hata machujo yake,
kikombe kile cha kunywea
kiwafanyacho watu kuyumbayumba.
18 Kati ya wana wote aliowazaa
hapakuwa na hata mmoja wa kumwongoza;
kati ya wana wote aliowalea
hapakuwa hata mmoja wa kumshika mkono.
19 Majanga haya mawili yamekuja juu yako:
ni nani awezaye kukufariji?
Maangamizi, uharibifu, njaa na upanga:
ni nani awezaye kukutuliza?
20 Wana wako wamezimia,
wamelala kwenye mwanzo wa kila barabara,
kama swala aliyenaswa kwenye wavu.
Wamejazwa na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu
na makaripio ya Mungu wako.
 
21 Kwa hiyo sikiliza hili, wewe uliyeteswa,
uliyelewa, lakini si kwa mvinyo.
22 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi wako,
Mungu wako, yeye ambaye huwatetea watu wake:
“Tazama, nimeondoa mkononi mwako
kikombe kilichokufanya uyumbayumbe;
kutoka kikombe hicho,
kikombe cha kunywa cha ghadhabu yangu,
kamwe hutakunywa tena.
23 Nitakiweka mikononi mwa watesi wako,
wale waliokuambia,
‘Anguka kifudifudi
ili tuweze kutembea juu yako.’
Ukaufanya mgongo wako kama ardhi,
kama njia yao ya kupita.”