Yakobo
1
Salamu
Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Isa Al-Masihi.
Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni.
Salamu.
Imani na hekima
Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Acheni saburi ikamilishe kazi yake, ili mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote. Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima, basi amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa. Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, linalopeperushwa na upepo na kutupwa huku na huko. Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana Isa. Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.
Umaskini na utajiri
Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa. 10 Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani. 11 Kwa maana jua kali huchomoza na kuyakausha majani ya mmea, nalo ua lake linaanguka, na uzuri wake unaharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake.
Kujaribiwa
12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji lile la uzima Mungu alilowaahidia wale wanaompenda.
13 Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. 15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa huzaa mauti.
16 Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike. 17 Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. 18 Kwa mapenzi yake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mazao ya kwanza katika viumbe vyake vyote.
Kusikia na kutenda
19 Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika. 20 Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. 21 Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.
22 Basi kuweni watendaji wa Neno, wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. 23 Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo 24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na husahau upesi jinsi alivyo. 25 Lakini yeye anayeangalia kwa makini katika sheria kamilifu iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau, bali akatenda alichosikia, basi atabarikiwa katika kile anachofanya.
26 Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake haifai kitu. 27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu, Baba*Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, ndiyo hii: ni kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

*1:27 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.