2
Onyo kuhusu upendeleo
Ndugu zangu, waumini katika imani ya Bwana wetu wa utukufu, Isa Al-Masihi, hawapaswi kuwa na upendeleo. Je, ikiwa mtu anakuja katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, na kisha akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa. Mkimpa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” je, hamjabagua kati yenu wenyewe na kuwa mahakimu wenye mawazo maovu?
Ndugu zangu, sikilizeni: Je, si Mungu huwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi ufalme aliowaahidi wale wanaompenda? Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani? Je, si wao wanalikufuru jina lile bora sana mliloitiwa?
Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko, isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema. Lakini mkiwapendelea watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa wakosaji. 10 Kwa maana mtu yeyote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote. 11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” alisema pia, “Usiue.” Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.
12 Hivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu yeyote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.
Imani na matendo
14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? 15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, 16 naye mmoja wenu akamwambia, “Nenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? 17 Vivyo hivyo, imani peke yake, kama haikuambatana na matendo, imekufa.
18 Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.”
Nioneshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo. 19 Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani wanaamini hivyo na kutetemeka.
20 Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu? 21 Je, Ibrahimu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaka madhabahuni? 22 Unaona jinsi imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda. 23 Kwa njia hiyo likatimizwa andiko lisemalo, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu. 24 Mnaona kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.
25 Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba: je, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? 26 Kama vile mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.