2
Malaika wa Mwenyezi Mungu huko Bokimu
1 Malaika wa Mwenyezi Mungu akakwea kutoka Gilgali hadi Bokimu, naye akasema, “Niliwapandisha kutoka Misri, na kuwaingiza katika nchi niliyoapa kuwapa baba zenu. Nikasema, ‘Kamwe sitalivunja agano langu nanyi. 2 Msifanye agano na watu wa nchi hii, bali mtabomoa madhabahu yao.’ Lakini ninyi hamkunitii mimi. Kwa nini mmefanya jambo hili? 3 Sasa basi ninawaambia kuwa sitawafukuza watoke kati yenu, ila watakuwa mitego kwenu, nayo miungu yao itakuwa tanzi kwenu.”
4 Malaika wa Mwenyezi Mungu alipomaliza kusema mambo haya kwa Waisraeli wote, watu wakalia kwa sauti kuu. 5 Wakapaita mahali pale Bokimu. Nao wakamtolea Mwenyezi Mungu sadaka.
Kifo cha Yoshua
6 Baada ya Yoshua kuwapa watu ruhusa waende zao, Waisraeli wakaenda kwenye urithi wao wenyewe ili kumiliki nchi yao. 7 Watu wakamtumikia Mwenyezi Mungu siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, wale waliokuwa wameona mambo makuu ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa ametenda kwa ajili ya Israeli.
8 Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mwenyezi Mungu, akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. 9 Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Heresi*Unajulikana pia kama Timnath-Sera(taz. Yoshua 19:50; 24:30). katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini mwa Mlima Gaashi.
10 Baada ya kizazi kile chote kukusanywa pamoja na baba zao, kikainuka kizazi kingine baada yao ambacho hakikumjua Mwenyezi Mungu, wala matendo yale aliyokuwa ametenda kwa ajili ya Waisraeli. 11 Kwa hiyo Waisraeli wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu na kuwatumikia Mabaali. 12 Wakamwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri. Wakaifuata na kuiabudu miungu mbalimbali ya mataifa yaliyowazunguka. Wakamkasirisha Mwenyezi Mungu, 13 kwa sababu walimwacha na kutumikia Baali na Maashtorethi. 14 Hivyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa wavamizi waliowateka nyara. Akawauza katika mikono ya adui zao pande zote, hivyo hawakuweza tena kuwazuia adui zao. 15 Wakati wowote Israeli walipotoka kwenda kupigana, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa kinyume nao ili awashinde, kama vile alivyokuwa amewaapia. Nao wakawa katika taabu kubwa.
16 Ndipo Mwenyezi Mungu akawainua waamuzi, ambao waliwaokoa kutoka mikononi mwa hao wavamizi. 17 Lakini hawakuwasikiliza hata waamuzi wao, bali walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine na kuiabudu. Waligeuka upesi na kuiacha njia ambayo baba zao waliiendea, yaani njia ya kutii amri za Mwenyezi Mungu. 18 Kila mara Mwenyezi Mungu alipowainulia mwamuzi, Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na huyo mwamuzi, naye aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao kwa kipindi chote alichoishi yule mwamuzi. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliwahurumia kwa sababu ya kilio chao cha huzuni kwa ajili ya wale waliokuwa wakiwatesa na kuwataabisha. 19 Lakini kila mara mwamuzi alipofariki, watu walirudia katika hali mbaya ya uovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine, ili kuitumikia na kuiabudu. Walikataa kuacha matendo yao maovu na njia zao za ukaidi.
20 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawakasirikia sana Israeli na kusema, “Kwa kuwa taifa hili limevunja agano lile nililofanya na baba zao na hawakunisikiliza, 21 mimi nami sitafukuza taifa lolote ambalo Yoshua aliliacha alipofariki. 22 Nitawatumia mataifa hao ili nipate kuwapima Israeli, nione kama wataishika njia ya Mwenyezi Mungu na kuenenda kwa njia hiyo jinsi baba zao walivyofanya.” 23 Mwenyezi Mungu alikuwa ameyaacha hayo mataifa yabaki; hakuyaondoa mara moja kwa kuyatia mikononi mwa Yoshua.