3
Mataifa yaliyobaki katika nchi
1 Haya ndio mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyaacha ili kuwajaribu Waisraeli wote ambao hawakushiriki vita yoyote huko Kanaani 2 (alifanya hivi ili tu kuwafundisha vita wazao wa Waisraeli ambao hawakuwa na uzoefu wa vita hapo awali): 3 watawala watano wa Wafilisti, pamoja na Wakanaani wote, Wasidoni, na Wahivi walioishi katika milima ya Lebanoni kuanzia Mlima wa Baal-Hermoni hadi Lebo-Hamathi. 4 Waliachwa ili kuwajaribu Waisraeli, kuona kama wangetii amri za Mwenyezi Mungu, alizokuwa amewapa baba zao kwa mkono wa Musa.
5 Waisraeli wakaishi miongoni mwa Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 6 Wakaoa binti za hao mataifa, na wakawatoa binti zao wenyewe waolewe na wana wa hao mataifa, na wakaitumikia miungu yao.
Othnieli
7 Waisraeli wakafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, wakamsahau Mwenyezi Mungu, Mungu wao, na kutumikia Mabaali na Maashera. 8 Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Israeli. Hivyo akawauza mikononi mwa Kushan-Rishathaimu mfalme wa Mesopotamia, nao Waisraeli wakamtumikia kwa muda wa miaka nane. 9 Waisraeli walipomlilia Mwenyezi Mungu, yeye akawainulia mkombozi, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu, ambaye aliwaokoa. 10 Roho wa Mwenyezi Mungu akaja juu yake; hivyo akawa mwamuzi wa Israeli, na akaenda vitani. Mwenyezi Mungu akamtia Kushan-Rishathaimu mfalme wa Mesopotamia mikononi mwa Othnieli, naye akamshinda. 11 Hivyo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arobaini, hadi Othnieli mwana wa Kenazi alipofariki.
Ehudi
12 Waisraeli wakafanya maovu mbele za Mwenyezi Mungu tena; na kwa kuwa walifanya maovu hayo, Mwenyezi Mungu akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli. 13 Egloni akawakusanya Waamoni na Waamaleki kwake, wakashambulia Israeli, na wakatwaa Mji wa Mitende*yaani Yeriko. 14 Waisraeli wakawa chini ya Egloni mfalme wa Moabu kwa muda wa miaka kumi na nane.
15 Waisraeli wakamlilia tena Mwenyezi Mungu, naye akawapa mkombozi: Ehudi, mtu wa shoto, mwana wa Gera Mbenyamini. Waisraeli wakatuma kwa Egloni mfalme wa Moabu ushuru kwa mkono wa Ehudi. 16 Basi Ehudi alikuwa ametengeneza upanga ukatao kuwili, ukiwa na urefu wa kama dhiraa moja†Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45., naye akaufunga upanga huo ndani ya nguo yake, kwenye paja lake la mkono wa kuume. 17 Akamkabidhi ushuru Egloni mfalme wa Moabu, aliyekuwa mtu mnene sana. 18 Baada ya Ehudi kumkabidhi ule ushuru, akawatuma wale watu waliokuwa wameubeba huo ushuru waende zao. 19 Ehudi akafuatana nao hadi kwenye sanamu za mawe karibu na Gilgali, ndipo yeye akarudi, akafika kwa Egloni na kusema, “Ee Mfalme, ninao ujumbe wa siri kwako.”
Mfalme akasema, “Nyamazeni kimya!” Nao wale waliomhudumia wote wakamwacha, wakatoka nje.
20 Ndipo Ehudi akamsogelea alipokuwa ameketi peke yake kwenye chumba cha juu cha jumba lake la kifalme la majira ya kiangazi, na kusema, “Ninao ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili yako.” Mfalme alipokuwa anainuka kutoka kiti chake, 21 Ehudi akaunyoosha mkono wake wa kushoto na kuufuta ule upanga aliokuwa ameufunga kwenye paja lake la kulia, akamdunga Mfalme Egloni tumboni mwake. 22 Hata mpini nao ukazama tumboni pamoja na upanga wenyewe, nao upanga ukatokea mgongoni mwake. Ehudi hakuuchomoa huo upanga, nayo mafuta yakashikamana juu ya upanga. 23 Ehudi akatoka nje barazani; akamfungia milango ya chumba cha juu, na kuifunga kwa funguo.
24 Baada yake kuondoka, watumishi wakaja na kupata milango ya chumba cha juu imefungwa kwa funguo. Wakasema, “Bila shaka anajisaidia chumba cha ndani.” 25 Wakangoja hadi wakawa na fadhaa, na wakati hakuifungua milango ya chumba, wakachukua funguo na kuifungua. Tazama, wakaona bwana wao amelala sakafuni, amekufa.
26 Walipokuwa wangali wanangoja, Ehudi akatoroka, akapita hapo kwenye sanamu ya kuchora kwenye mawe na kukimbilia Seira. 27 Alipofika huko, akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakateremka pamoja naye kutoka vilimani, yeye akiwa anawaongoza.
28 Akawaagiza, “Nifuateni, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewatia Moabu, adui zenu, mikononi mwenu.” Kwa hiyo wakateremka wakamfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kuelekea Moabu, wala hawakumwacha mtu yeyote kuvuka. 29 Wakati huo wakawaua Wamoabu wapatao elfu kumi wenye nguvu na mashujaa; hakuna yeyote aliyetoroka. 30 Siku ile Moabu wakashindwa na Israeli, nayo nchi ikawa na amani kwa miaka themanini.
Shamgari
31 Baada ya Ehudi akaja Shamgari mwana wa Anathi, aliyewapiga Wafilisti mia sita kwa fimbo ya ng’ombe. Naye pia akawaokoa Waisraeli.