4
Debora
Baada ya Ehudi kufa, Waisraeli wakafanya tena maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Hivyo Mwenyezi Mungu akawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori. Jemadari wa jeshi lake alikuwa Sisera, aliyeishi huko Haroshethi-Hagoyimu*yaani Haroshethi ya Mataifa. Kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya vita ya chuma yapatayo mia tisa, naye alikuwa amewatesa Waisraeli kwa ukatili kwa muda wa miaka ishirini, Waisraeli wakamlilia Mwenyezi Mungu wakaomba msaada.
Debora, nabii mwanamke, mkewe Lapidothi, ndiye alikuwa anaamua Israeli wakati ule. Debora alikuwa akiketi chini ya Mtende wa Debora uliokuwa kati ya Rama na Betheli katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakaja kwake ili awaamue. Akatuma wamwite Baraka mwana wa Abinoamu kutoka Kedeshi huko Naftali na kumwambia, “Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, anakuagiza: ‘Nenda, chukua wanaume elfu kumi toka Naftali na Zabuloni, mwende Mlima Tabori. Nitamshawishi Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, pamoja na magari yake ya vita na jeshi lake, hadi Mto Kishoni na kumtia mikononi mwako.’ ”
Baraka akamwambia, “Ukienda pamoja nami nitaenda, lakini usipoenda pamoja nami, sitaenda.”
Debora akamwambia, “Hakika nitaenda pamoja nawe, lakini njia unayoiendea haitakupa heshima wewe, kwa kuwa Mwenyezi Mungu atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Hivyo Debora akaenda pamoja na Baraka hadi Kedeshi, 10 ambapo Baraka aliwaita Zabuloni na Naftali. Watu elfu kumi wakamfuata Baraka, na Debora pia akaenda naye.
11 Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wale wengine, yaani wazao wa Hobabu, mkwewe Musa, naye akapiga hema lake karibu na ule mti mkubwa wa mwaloni ulio Saananimu, karibu na Kedeshi.
12 Sisera alipoambiwa kuwa Baraka mwana wa Abinoamu alikuwa amepanda Mlima Tabori, 13 Sisera akakusanya magari yake ya vita ya chuma mia tisa, na watu wote waliokuwa pamoja naye, kuanzia Haroshethi-Hagoyimu hadi Mto wa Kishoni.
14 Ndipo Debora akamwambia Baraka, “Nenda! Hii ndiyo siku ambayo Mwenyezi Mungu amemtia Sisera mikononi mwako. Je, Mwenyezi Mungu hakukutangulia mbele yako?” Hivyo Baraka akashuka kutoka Mlima Tabori, akifuatwa na watu elfu kumi. 15 Mwenyezi Mungu akamfadhaisha Sisera na magari yake ya vita yote, pamoja na jeshi lake lote kwa upanga mbele ya Baraka, naye Sisera akaliacha gari lake la vita na kukimbia kwa miguu. 16 Lakini Baraka akafuata magari ya vita pamoja na jeshi hadi Haroshethi-Hagoyimu. Jeshi lote la Sisera likaanguka kwa upanga, wala hakuna hata mtu mmoja aliyesalia.
17 Sisera, hata hivyo, akakimbia kwa miguu hadi kwenye hema la Yaeli, mkewe Heberi, Mkeni, kwa sababu palikuwa na uhusiano wa kirafiki kati ya Yabini mfalme wa Hazori na ukoo wa Heberi, Mkeni.
18 Yaeli akaenda kumlaki Sisera na kumwambia, “Karibu, bwana wangu, karibu ingia ndani kabisa. Usiogope.” Basi Sisera akaingia ndani ya hema la Yaeli, naye akamfunika kwa blanketi nene.
19 Akamwambia, “Nina kiu, tafadhali nipe maji ya kunywa.” Ndipo akafungua kiriba cha maziwa na kumpa akanywa, kisha akamfunika.
20 Naye Sisera akamwambia, “Simama mlangoni pa hema na mtu yeyote akija na kukuuliza, ‘Je, kuna mtu yeyote hapa?’ sema, ‘Hapana.’ ”
21 Lakini Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akachukua nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akiwa amelala usingizi kwa kuchoka. Akakipigilia kile kigingi kwenye paji la uso wake, kikapenya hata kuingia ardhini, naye akafa.
22 Baraka akakaribia akimfuatia Sisera, Yaeli akatoka kumlaki. Akamwambia, “Njoo, nitakuonesha mtu unayemtafuta.” Hivyo wakaingia ndani ya hema, na tazama, Sisera alikuwa amelala humo akiwa amekufa, na hicho kigingi cha hema kikiwa kimepigiliwa kupitia paji la uso wake.
23 Basi siku ile Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani, mbele ya Israeli. 24 Nao mkono wa Waisraeli ukaendelea kuwa na nguvu zaidi na zaidi dhidi ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hadi wakamwangamiza.

*4:2 yaani Haroshethi ya Mataifa