6
Gideoni
Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu akawatia mikononi mwa Wamidiani kwa muda wa miaka saba. Kwa kuwa Wamidiani walikuwa na nguvu juu yao, Waisraeli walijitengenezea maficho milimani, kwenye mapango, na katika ngome. Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao. Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ng’ombe au punda. Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia wao; wakavamia nchi ili kuiharibu. Wamidiani wakaifanya Israeli kuwa maskini sana, hata Waisraeli wakamlilia Mwenyezi Mungu kumwomba msaada.
Waisraeli walipomlilia Mwenyezi Mungu kwa sababu ya Wamidiani, Mwenyezi Mungu akawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa. Nikawaokoa kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu, nami nikawapa ninyi nchi yao. 10 Nikawaambia, ‘Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”
11 Malaika wa Mwenyezi Mungu akaja akaketi chini ya mwaloni ulio Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi Mwabiezeri, pale Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione. 12 Malaika wa Mwenyezi Mungu alipomtokea Gideoni, akamwambia, “Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe, ewe shujaa mwenye nguvu.”
13 Gideoni akajibu, “Nisamehe, Ee Bwana wangu. Kama Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi yale matendo yake makuu ambayo baba zetu walitusimulia juu yake waliposema, ‘Je, Mwenyezi Mungu hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa Mwenyezi Mungu ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”
14 Mwenyezi Mungu akamgeukia na kusema “Nenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”
15 Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”
16 Mwenyezi Mungu akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”
17 Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonesha kuwa kweli ni wewe unayesema nami. 18 Tafadhali nakuomba usiondoke hapa hadi nitakaporudi, nilete sadaka yangu na kuiweka mbele yako.”
Naye Mwenyezi Mungu akamwambia, “Nitangoja hadi utakaporudi.”
19 Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja*Efa moja ni sawa na lita 22. ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mwaloni, akampa.
20 Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo. 21 Malaika wa Mwenyezi Mungu akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa Mwenyezi Mungu akatoweka machoni pake. 22 Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa Mwenyezi Mungu, akapaza sauti, akasema, “Ole wangu, Bwana Mungu Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Mwenyezi Mungu uso kwa uso!”
23 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”
24 Hivyo Gideoni akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu mahali pale na kupaita Yehova-Shalomumaana yake Mwenyezi Mungu ni Amani. Hata leo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.
25 Usiku ule ule Mwenyezi Mungu akamwambia, “Mchukue ng’ombe dume wa baba yako, yule wa pili mwenye miaka saba, ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate nguzo ya Ashera iliyo karibu nayo. 26 Kisha mjengee Mwenyezi Mungu, Mungu wako, madhabahu kwa taratibu zake juu ya mwamba katika ngome hii. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”
27 Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.
28 Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa, na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa, na yule ng’ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu iliyojengwa upya!
29 Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?”
Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.”
30 Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”
31 Lakini Yoashi akaambia umati wa watu waliomzunguka wakiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Yeyote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.” 32 Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake.
33 Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ng’ambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli. 34 Ndipo Roho wa Mwenyezi Mungu akamjia Gideoni, naye Gideoni akapiga tarumbeta kuwaita Waabiezeri ili wamfuate. 35 Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao.
36 Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi: 37 tazama, nitaweka manyoya ya kondoo kwenye sakafu ya kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya manyoya tu, na ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.” 38 Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akayakamua yale manyoya yenye umande, yakatoka maji kiasi cha kujaa bakuli.
39 Kisha Gideoni akamwambia Mwenyezi Mungu, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa manyoya haya. Wakati huu uyafanye manyoya kuwa kavu, na ardhi yote ifunikwe na umande.” 40 Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Manyoya yakawa kavu, na ardhi yote ikafunikwa na umande.

*6:19 Efa moja ni sawa na lita 22.

6:24 maana yake Mwenyezi Mungu ni Amani