7
Gideoni awashinda Wamidiani
1 Ndipo Yerub-Baali (yaani Gideoni) na lile jeshi lililokuwa pamoja naye, wakaondoka asubuhi na mapema na kupiga kambi kando ya chemchemi ya Harodi. Kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini mwao katika bonde, karibu na kilima cha More. 2 Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Jeshi lililo pamoja nawe ni kubwa sana kwangu kuwatia Wamidiani mikononi mwao, Israeli asije akajisifu juu yangu, akisema, ‘Mkono wangu ndio uliniokoa.’ 3 Kwa hiyo sasa tangaza jeshi lote likiwa linasikia, kwamba: ‘Yeyote anayeogopa na kutetemeka, yeye na arudi nyumbani, aondoke katika Mlima Gileadi.’ ” Hivyo, watu elfu ishirini na mbili wakarudi nyumbani, wakabaki elfu kumi.
4 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Idadi ya jeshi bado ni kubwa. Wapeleke kwenye maji, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako. Nikikuambia, ‘Huyu ataenda pamoja nawe,’ yeye ataenda; lakini nikisema, ‘Huyu hataenda pamoja nawe,’ yeye hataenda.”
5 Gideoni akalipeleka lile jeshi kwenye maji, naye Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Watenganishe watakaoramba maji kwa ulimi kama mbwa, na wale watakaopiga magoti ili kunywa.” 6 Waliokunywa kwa kuramba maji kutoka mikononi mwao walikuwa watu mia tatu. Wengine wote walipiga magoti ili kunywa.
7 Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Kupitia hao watu mia tatu walioramba maji nitawaokoa ninyi, nami nitawatia Wamidiani mkononi mwako. Waache hao watu wengine wote warudi kila mmoja nyumbani mwake.” 8 Hivyo Gideoni akawaruhusu wale Waisraeli wengine kila mmoja aende kwenye hema lake. Akabakia na wale mia tatu, nao wakachukua vyakula na tarumbeta za wenzao.
Basi kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake bondeni. 9 Usiku ule ule Mwenyezi Mungu akamwambia Gideoni, “Ondoka, ushuke ushambulie kambi, kwa kuwa nimeitia mkononi mwako. 10 Lakini kama unaogopa kushambulia, shuka kambini pamoja na mtumishi wako Pura, 11 nawe sikiliza wanayosema. Hatimaye, utatiwa moyo kushambulia kambi.” Basi yeye na Pura, mtumishi wake, wakashuka na kuwafikia walinzi wa mbele wa kambi. 12 Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia wao hawangehesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.
13 Gideoni alifika mara tu mtu mmoja alipokuwa akimweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Tazama, niliota ndoto, mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukaipiga hema kwa nguvu, na kusababisha hema hilo kupinduka na kuporomoka.”
14 Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine isipokuwa upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.”
15 Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akasujudu na kuabudu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! Mwenyezi Mungu amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.” 16 Akawagawa wale watu mia tatu katika makundi matatu, akawakabidhi tarumbeta mikononi mwao wote, na mitungi mitupu, na mienge ikawekwa ndani yake.
17 Akawaambia, “Nitazameni, fanyeni kama nitakavyofanya. Nitakapofika mwisho wa kambi, mfanye kama nitakavyofanya. 18 Mimi na wote walio pamoja nami tutakapopiga tarumbeta zetu, ninyi nanyi pigeni tarumbeta pande zote za kambi na mpige kelele, mseme, ‘Upanga wa Mwenyezi Mungu na wa Gideoni.’ ”
19 Gideoni na wale watu mia moja waliokuwa pamoja naye wakafika mwisho wa kambi usiku mwanzoni mwa zamu ya kati, mara tu walipokuwa wamebadili zamu. Wakapiga zile tarumbeta zao, na kuvunja ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. 20 Yale makundi matatu wakapiga tarumbeta na kuvunja mitungi. Wakashika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga. Wakapaza sauti zao, wakisema, “Upanga wa Mwenyezi Mungu, na wa Gideoni!” 21 Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote, Wamidiani wote wakakimbia, huku wakipiga kelele.
22 Walipozipiga zile tarumbeta mia tatu, Mwenyezi Mungu akafanya watu katika kambi yote kugeukiana kila mmoja na mwenziwe kwa upanga. Jeshi likakimbia hadi Beth-Shita kuelekea Serera*au Seretha, hadi mpakani mwa Abel-Mehola karibu na Tabathi. 23 Wanaume Waisraeli wakaitwa kutoka Naftali, Asheri na Manase yote, nao wakawafuatia Wamidiani. 24 Gideoni akatuma wajumbe katika nchi yote ya vilima ya Efraimu, akisema, “Teremkeni dhidi ya Wamidiani na mkazuie vivuko vya maji mbele yao hadi Beth-Bara na pia Yordani.”
Hivyo wanaume wote wa Efraimu wakakutanika pamoja na kuzingira vivuko vya maji mbele yao hadi Beth-Bara na pia Yordani. 25 Wakawakamata Orebu na Zeebu, wakuu wawili wa Midiani. Wakamuua Orebu pale penye mwamba wa Orebu, na Zeebu wakamuua pale penye shinikizo la kukamulia zabibu la Zeebu. Wakawafuatia Wamidiani na kuleta vichwa vya Orebu na Zeebu kwa Gideoni, huko ng’ambo ya Yordani.