8
Ushindi wa Gideoni na kulipiza kisasi
Basi Waefraimu wakamuuliza Gideoni, “Mbona umetutenda hivi? Kwa nini hukutuita ulipoenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali sana.
Gideoni akawajibu, “Nilichofanya mimi ni nini kulinganisha na kile ninyi mlichofanya? Je, kuokoa masazo ya zabibu za Efraimu si bora kuliko mavuno kamili ya zabibu ya Abiezeri? Mungu amewatia Orebu na Zeebu, hao viongozi wa Wamidiani, mikononi mwenu. Je, mimi niliweza kufanya nini kulinganisha na mlichofanya ninyi?” Aliposema hili, hasira yao dhidi yake ikatulia.
Gideoni pamoja na watu wake mia tatu, wakiwa wamechoka sana lakini bado wakiwafuatia, wakafika Yordani na kuuvuka. Akawaambia wanaume wa Sukothi, “Tafadhali lipatieni jeshi langu mikate, kwa maana wamechoka, nami ningali ninawafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.”
Lakini viongozi wa Sukothi wakasema, “Je, tayari umewakamata Zeba na Salmuna ili tulipatie jeshi lako mikate?”
Gideoni akajibu, “Kwa ajili ya hilo tu, Mwenyezi Mungu atakapowatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, nitaichana nyama ya miili yenu kwenye miiba ya nyikani na kwenye michongoma.”
Kutoka hapo alikwea hadi Penieli na kutoa ombi lile lile, lakini nao wanaume wa Penieli wakamjibu kama wanaume wa Sukothi walivyokuwa wamemjibu. Hivyo akawaambia wanaume wa Penieli, “Nitakaporudi kwa ushindi, nitaubomoa mnara huu.”
10 Wakati huu Zeba na Salmuna walikuwa Karkori, wakiwa na jeshi la watu wapatao elfu kumi na tano waliokuwa wamesalia wa mataifa ya mashariki, kwa kuwa watu wapatao elfu mia moja na ishirini wenye panga walikuwa wameuawa. 11 Basi Gideoni akakwea kwa njia ya wafugaji wahamaji mashariki mwa Noba na Yogbeha, na kulishambulia jeshi ambalo halikushuku lolote. 12 Zeba na Salmuna, hao wafalme wawili wa Midiani, wakakimbia lakini yeye Gideoni akawafuata na kuwakamata, akalishinda hilo jeshi lao lote kabisa.
13 Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani kupitia Mwinuko wa Heresi. 14 Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumuuliza maswali, naye yule kijana akamwandikia majina ya viongozi sabini na saba wa Sukothi, ambao ni wazee wa mji. 15 Ndipo Gideoni akaja na kuwaambia wanaume wa Sukothi, “Tazameni Zeba na Salmuna mlionisimanga kwa ajili yao mkisema, ‘Je, tayari umewakamata Zeba na Salmuna ili tulipatie jeshi lako mikate?’ ” 16 Akawachukua hao wazee wa mji, na kuwaadhibu wanaume wa Sukothi kwa kuwachapa kwa miiba na michongoma ya nyikani. 17 Pia akaubomoa mnara wa Penieli na kuwaua wanaume wa huo mji.
18 Kisha akawauliza Zeba na Salmuna, “Ni wanaume wa aina gani mliowaua huko Tabori?”
Wakajibu, “Ni wanaume kama wewe, kila mmoja wao akiwa anafanana na mwana wa mfalme.”
19 Gideoni akajibu, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu hasa. Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, kama mngekuwa mmewaacha hai, mimi nisingewaua ninyi.” 20 Akamgeukia Yetheri, mwanawe mzaliwa wa kwanza, akasema, “Waue hawa!” Lakini Yetheri hakuufuta upanga wake, kwa sababu aliogopa, kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo tu.
21 Zeba na Salmuna wakasema, “Njoo ufanye hivyo wewe mwenyewe. ‘Alivyo mwanaume, ndivyo zilivyo nguvu zake.’ ” Hivyo, Gideoni akajitokeza na kuwaua, naye akayaondoa mapambo kwenye shingo za ngamia wao.
Kizibau cha Gideoni
22 Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Ututawale, wewe, mwanao, na mjukuu wako, kwa kuwa umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.”
23 Lakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitawatawala ninyi, wala mwanangu hatawatawala. Mwenyezi Mungu ndiye atakayewatawala ninyi.” 24 Naye akasema, “Ninalo ombi moja, kwamba kila mmoja wenu anipatie kipuli kutoka fungu lake la nyara.” (Ilikuwa desturi ya Waishmaeli kuvaa vipuli vya dhahabu.)
25 Wakajibu, “Tutafurahi kuvitoa.” Hivyo wakatanda vazi chini na kila mwanaume akatupia juu yake pete kutoka fungu lake la nyara. 26 Uzito wa pete za dhahabu alizoomba ulikuwa shekeli elfu moja na mia saba*Shekeli 1,700 ni sawa na kilo 19.5., bila kuhesabu mapambo mengine, vidani, na mavazi ya zambarau yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani, au mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia wao. 27 Gideoni akatengeneza kizibau kwa kutumia ile dhahabu, ambacho alikiweka katika mji wake, yaani Ofra. Waisraeli wote wakafanya uasherati kwa kukiabudu huko, nacho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake.
28 Hivyo Midiani wakashindwa mbele ya Waisraeli, nao hawakuinua vichwa vyao tena. Wakati wa siku za uhai wa Gideoni, nchi ikafurahia amani miaka arobaini.
Kifo cha Gideoni
29 Yerub-Baali mwana wa Yoashi akarudi kwenda kuishi katika nyumba yake. 30 Alikuwa na wana sabini wa kwake mwenyewe, kwa kuwa alikuwa na wake wengi. 31 Suria wake, aliyekuwa anaishi huko Shekemu, pia alimzalia mwana, akamwita jina Abimeleki. 32 Gideoni mwana wa Yoashi akafa akiwa na umri mzuri wa uzee, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake huko Ofra ya Waabiezeri.
33 Mara tu alipofariki Gideoni, Waisraeli wakarudia hali ya uovu na kufanya uasherati kwa kuabudu Mabaali. Wakamsimamisha Baal-Berithi kuwa mungu wao na 34 wala hawakumkumbuka Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyewaokoa kutoka mikononi mwa adui zao wote kutoka kila upande. 35 Pia wakashindwa kuitendea mema jamaa ya Yerub-Baali (yaani Gideoni) kwa ajili ya mambo yote mema aliyokuwa amefanyia Israeli.

*8:26 Shekeli 1,700 ni sawa na kilo 19.5.