17
Sanamu za Mika
Palikuwa na mtu aliyeitwa Mika kutoka nchi ya vilima ya Efraimu. Akamwambia mama yake, “Zile shekeli elfu moja na mia moja*Shekeli 1,100 ni sawa na kilo 13. za fedha zilizochukuliwa kwako, ambazo nilisikia ukizinenea maneno ya laana, hizi hapa; mimi ndiye niliyezichukua.”
Ndipo mama yake akamwambia, “Mwenyezi Mungu na akubariki, mwanangu.”
Alipozirudisha zile shekeli elfu moja na mia moja za fedha kwa mama yake, mama yake akamwambia, “Mimi nimeiweka fedha hii wakfu kwa Mwenyezi Mungu ili mwanangu atengeneze sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu. Mimi nitakurudishia wewe.”
Hivyo akamrudishia mama yake ile fedha, naye mama yake akachukua shekeli mia mbiliShekeli 200 za fedha ni sawa na kilo 2.3 za fedha. za hiyo fedha na kumpa mfua fedha, ambaye aliifanyiza kinyago na sanamu. Navyo vikawekwa ndani ya nyumba ya Mika.
Basi Mika alikuwa na mahali pa ibada za sanamu. Akatengeneza kizibau, pamoja na miungu ya nyumbani, na kumweka mmoja wa wanawe kuwa kuhani wake. Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme; kila mtu alifanya alivyoona ni vyema machoni pake.
Palikuwa na kijana Mlawi kutoka Bethlehemu ya Yuda, aliyekuwa akiishi miongoni mwa watu wa kabila la Yuda. Huyu kijana akatoka mji huo wa Bethlehemu ya Yuda na kutafuta mahali pengine pa kuishi. Alipokuwa akisafiri, akafika nyumbani kwa Mika katika nchi ya vilima ya Efraimu.
Mika akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?”
Akamjibu, “Mimi ni Mlawi kutoka Bethlehemu ya Yuda, ninatafuta mahali pa kuishi.”
10 Ndipo Mika akamwambia, “Ishi pamoja nami, uwe baba yangu na kuhani wangu, nami nitakupa shekeli kumiShekeli 10 za fedha ni sawa na gramu 115 za fedha. za fedha kila mwaka, pamoja na nguo na chakula.” 11 Hivyo yule Mlawi akakubali kuishi pamoja na Mika, naye akawa kama mmoja wa wanawe. 12 Basi Mika akamweka wakfu huyo kijana Mlawi, naye huyo akawa kuhani wake na kuishi nyumbani mwake. 13 Mika akasema, “Sasa najua Mwenyezi Mungu atanitendea mema, kwa kuwa Mlawi huyu amekuwa kuhani wangu.”

*17:2 Shekeli 1,100 ni sawa na kilo 13.

17:4 Shekeli 200 za fedha ni sawa na kilo 2.3 za fedha.

17:10 Shekeli 10 za fedha ni sawa na gramu 115 za fedha.