18
Wadani wahamia Laishi
1 Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme.
Katika siku hizo, watu wa kabila la Dani walikuwa wanatafuta mahali pao wenyewe pa kuishi, kwa sababu walikuwa hawajafika kwenye urithi wao miongoni mwa makabila ya Israeli. 2 Hivyo Wadani wakatuma mashujaa watano kutoka Sora na Eshtaoli ili kupeleleza nchi na kuichunguza. Hawa mashujaa waliwakilisha koo zao zote. Waliwaambia, “Nendeni mkaichunguze hiyo nchi.”
Wanaume hao wakaingia katika nchi ya vilima ya Efraimu, wakafika nyumba ya Mika, ambako walilala usiku huo. 3 Walipofika karibu na nyumba ya Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi; hivyo wakaingia humo na kumuuliza, “Ni nani aliyekuleta hapa? Unafanya nini mahali hapa? Kwa nini uko hapa?”
4 Akawaeleza yale Mika aliyomtendea, akasema, “Ameniajiri, nami ni kuhani wake.”
5 Kisha wakamwambia, “Tafadhali tuulizie kwa Mungu kama safari yetu itafanikiwa.”
6 Yule kuhani akawajibu, “Nendeni kwa amani. Safari yenu ina kibali cha Mwenyezi Mungu.”
7 Basi hao wanaume watano wakaondoka na kufika Laishi, mahali ambapo waliwakuta watu wanaishi salama, kama Wasidoni, kwa amani na utulivu. Nchi yao haikupungukiwa kitu, hivyo wakastawi. Pia walikaa mbali sana na Wasidoni, wala hawakushughulika na mtu yeyote.
8 Waliporudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, ndugu zao wakawauliza, “Mlionaje mambo huko?”
9 Wakajibu, “Twendeni, tukawavamie! Tumeona kuwa nchi ni nzuri sana. Je, hamtafanya chochote? Msisite kupanda ili kuimiliki. 10 Mtakapofika huko, mtawakuta watu walio salama, na nchi kubwa ambayo Mungu ameitia mikononi mwenu, isiyopungukiwa kitu chochote duniani.”
11 Ndipo wanaume mia sita kutoka ukoo wa Wadani, waliojifunga silaha za vita, wakaondoka Sora na Eshtaoli. 12 Walipokuwa wakisafiri wakapiga kambi huko Kiriath-Yearimu katika Yuda. Hii ndiyo sababu sehemu ya magharibi ya Kiriath-Yearimu inaitwa Mahane-Dani*yaani Kambi ya Dani hadi leo. 13 Kutoka hapo wakaenda hadi nchi ya vilima ya Efraimu na kufika katika nyumba ya Mika.
14 Ndipo wale wanaume watano waliopeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mnajua kuwa katika mojawapo ya nyumba hizi kuna kizibau, miungu ya nyumbani, sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Sasa basi, fikirini mtakalofanya.” 15 Basi wakaelekea huko, wakafika kwa yule kijana Mlawi, katika nyumba ya Mika, wakamsalimu. 16 Wale Wadani mia sita, wakiwa wamejifunga silaha, wakasimama penye ingilio la lango. 17 Wale watu watano walioenda kupeleleza nchi wakaingia ndani na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, kile kizibau, na ile miungu ya nyumbani, na ile sanamu ya kusubu, wakati yule kuhani akiwa amesimama pale penye ingilio la lango pamoja na wale watu mia sita waliojifunga silaha.
18 Hao watu walipoingia katika nyumba ya Mika na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, kile kizibau, na ile miungu ya nyumbani, na ile sanamu ya kusubu, yule kuhani akawauliza, “Mnafanya nini?”
19 Wakamjibu, “Nyamaza! Weka mkono wako juu ya kinywa chako na ufuatane nasi, uwe baba yetu na kuhani wetu. Si ni afadhali utumikie kabila na ukoo katika Israeli kama kuhani kuliko kumtumikia mtu mmoja na watu wa nyumbani mwake?” 20 Yule kuhani akafurahi. Akachukua kile kizibau, ile miungu ya nyumbani, na sanamu ya kuchonga, naye akaenda pamoja na wale watu. 21 Ndipo wakageuka na kuondoka, wakiwatanguliza mbele watoto wao wadogo, mifugo na mali yao.
22 Walipokuwa wamefika mbali toka nyumbani kwa Mika, watu walioishi karibu na Mika walikusanywa pamoja, nao wakawakimbiza Wadani. 23 Walipofuatilia huku wakipiga kelele, Wadani wakageuka, wakamwambia Mika, “Una nini wewe hata ukawaita watu waje kupigana nasi?”
24 Akawajibu, “Mmechukua miungu niliyoitengeneza, mkamchukua kuhani wangu, nanyi mkaondoka. Nimebaki na nini kingine? Mnawezaje kuniuliza, ‘Una nini wewe?’ ”
25 Wadani wakamjibu, “Usibishane nasi, la sivyo watu wenye hasira watakushambulia, nawe na watu wa nyumbani mwako mtapoteza maisha yenu.” 26 Basi Wadani wakaenda zao, naye Mika alipoona kuwa wana nguvu kuliko yeye, akageuka na kurudi nyumbani mwake.
27 Kisha wakachukua vitu vile Mika alikuwa amevitengeneza, na kuhani wake, wakaendelea hadi Laishi, dhidi ya watu walioishi na amani na utulivu. Wakawashambulia kwa upanga na kuuteketeza mji wao. 28 Hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa, kwa kuwa waliishi mbali na Sidoni, na hawakuwa na ushirikiano na mtu mwingine yeyote. Mji huo ulikuwa kwenye bonde karibu na Beth-Rehobu.
Wadani wakaujenga upya huo mji na kuishi humo. 29 Wakauita ule mji Dani kwa kufuata jina la baba yao aliyezaliwa na Israeli, ingawa mji huo uliitwa Laishi hapo awali. 30 Kule Wadani wakajisimamishia ile sanamu ya kuchonga, naye Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa pamoja na wanawe walikuwa makuhani kwa kabila la Dani hadi nchi hiyo ilipotekwa. 31 Wakaendelea kuiabudu ile sanamu ambayo Mika alizitengeneza, wakati wote ule nyumba ya Mungu ilikuwa huko Shilo.