14
Ukame, njaa na upanga
1 Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu kwa Yeremia kuhusu ukame:
2 “Yuda anaomboleza,
kudhoofika kwa miji yake;
wanaomboleza kwa ajili ya nchi,
nacho kilio kinapanda kutoka Yerusalemu.
3 Wakuu wanawatuma watumishi wao maji;
nao wanakwenda visimani
lakini huko hakuna maji.
Wanarudi na vyombo bila maji;
wakiwa na hofu na kukata tamaa,
wanafunika vichwa vyao.
4 Ardhi imepasuka nyufa
kwa sababu hakuna mvua katika nchi;
wakulima wana hofu
na wanafunika vichwa vyao.
5 Hata kulungu kondeni
anaacha kinda lake lililotoka kutotolewa
kwa sababu hakuna majani.
6 Punda-mwitu wanasimama juu ya miinuko iliyo kame
na kutweta kama mbweha;
macho yao yanakosa nguvu za kuona
kwa sababu ya kukosa malisho.”
7 Ingawa dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu,
Ee Mwenyezi Mungu, tenda jambo kwa ajili ya jina lako.
Kwa kuwa kukengeuka kwetu ni kukubwa,
nasi tumetenda dhambi dhidi yako.
8 Ee Tumaini la Israeli,
Mwokozi wake wakati wa taabu,
kwa nini unakuwa kama mgeni katika nchi,
kama msafiri anayekaa kwa usiku mmoja tu?
9 Mbona unakuwa kama mtu aliyeshtukizwa,
kama shujaa asiye na uwezo wa kuokoa?
Wewe uko katikati yetu, Ee Mwenyezi Mungu,
nasi tunaitwa kwa jina lako;
usituache!
10 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu watu hawa:
“Wanapenda sana kutangatanga,
hawaizuii miguu yao.
Hivyo Mwenyezi Mungu hawakubali;
sasa ataukumbuka uovu wao
na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.”
11 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Usiombe kwa ajili ya mafanikio ya watu hawa. 12 Ingawa wanafunga, sitasikiliza kilio chao; hata wakitoa dhabihu za kuteketezwa na dhabihu za nafaka, sitazikubali. Badala yake, nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”
13 Lakini nikasema, “Aa, Bwana Mungu Mwenyezi, manabii wanaendelea kuwaambia, ‘Hamtaona upanga wala kukabiliwa na njaa. Naam, nitawapa amani ya kudumu mahali hapa.’ ”
14 Ndipo Mwenyezi Mungu akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwachagua, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, uaguzi usio na faida, udanganyifu wa mioyo yao, na ubatili. 15 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu manabii wanaotabiri kwa jina langu: Mimi sikuwatuma, lakini wanasema, ‘Hakuna upanga wala njaa itakayoigusa nchi hii.’ Manabii hao hao watakufa kwa upanga na njaa. 16 Nao watu hao wanaowatabiria watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu kwa sababu ya njaa na upanga. Hapatakuwa na mtu wa kuwazika wao au wake zao, watoto wao wa kiume au wa kike. Nitawamwagia maafa wanayostahili.
17 “Nena nao neno hili:
“ ‘Macho yangu na yatiririkwe na machozi
usiku na mchana bila kukoma;
kwa kuwa binti yangu aliye bikira, yaani watu wangu,
amepata jeraha baya,
pigo la kuangamiza.
18 Ninapokwenda shambani,
ninaona wale waliouawa kwa upanga;
ninapokwenda mjini,
huko ninaona maangamizi ya njaa.
Nabii na kuhani kwa pamoja
wameenda katika nchi wasiyoijua.’ ”
19 Je, umemkataa Yuda kabisa?
Umemchukia Sayuni kabisa?
Kwa nini umetuumiza
hata hatuwezi kuponyeka?
Tulitarajia amani,
lakini hakuna jema lililotujia;
tulitarajia wakati wa kupona
lakini kuna hofu kuu tu.
20 Ee Mwenyezi Mungu, tunatambua uovu wetu
na kosa la baba zetu;
kweli tumetenda dhambi dhidi yako.
21 Kwa ajili ya jina lako usituchukie kabisa;
usikidharau kiti chako cha enzi kilichotukuka.
Kumbuka agano lako nasi
na usilivunje.
22 Je, kuna sanamu batili yoyote ya mataifa
iwezayo kuleta mvua?
Je, anga peke yake zinaweza kuleta mvua?
La hasha! Ni wewe peke yako,
Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.
Kwa hiyo tumaini letu liko kwako,
kwa kuwa wewe ndiwe ufanyaye haya yote.