15
Adhabu isiyoepukika
1 Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia: “Hata kama Musa na Samweli wangesimama mbele zangu, moyo wangu usingewaelekea watu hawa. Waondoe mbele za macho yangu! Waache waende! 2 Nao wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“ ‘Wale waliowekwa kwa ajili ya kufa, na wafe;
waliowekewa kufa kwa upanga, kwa upanga;
waliowekewa kufa kwa njaa, kwa njaa;
na waliowekewa kupelekwa uhamishoni,
wapelekwe uhamishoni.’ ”
3 Mwenyezi Mungu asema, “Nitatuma aina nne za waangamizi: upanga ili kuua, mbwa ili kukokota mbali, ndege wa angani na wanyama wa nchi ili wale na waangamize. 4 Nitawafanya wawe machukizo kwa falme zote za dunia kwa sababu ya kile alichofanya Manase mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda huko Yerusalemu.
5 “Ni nani atakayekuhurumia, ee Yerusalemu?
Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako?
Ni nani atakayesimama ili kuuliza
kuhusu hali yako?
6 Umenikataa mimi,” asema Mwenyezi Mungu.
“Unazidi kukengeuka.
Hivyo nitanyoosha mkono wangu juu yako na kukuangamiza,
siwezi kuendelea kukuonea huruma.
7 Nitawapepeta kwa ungo
kwenye malango ya miji ya nchi.
Nitaleta msiba na maangamizi juu ya watu wangu,
kwa maana hawajabadili njia zao.
8 Nitawafanya wajane wao kuwa wengi
kuliko mchanga wa bahari.
Wakati wa adhuhuri nitamleta mwangamizi
dhidi ya mama wa vijana wao wa kiume;
kwa ghafula nitaleta juu yao
maumivu makuu na hofu kuu.
9 Mama mwenye watoto saba atazimia
na kupumua pumzi yake ya mwisho.
Jua lake litatua kukiwa bado mchana,
atatahayarika na kufedheheka.
Wale wote waliobaki nitawaua kwa upanga
mbele ya adui zao,”
asema Mwenyezi Mungu.
10 Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa,
mtu ambaye ulimwengu wote
unashindana na kugombana naye!
Sikukopa wala sikukopesha,
lakini kila mmoja ananilaani.
11 Mwenyezi Mungu akasema,
“Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema,
hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada
nyakati za maafa na nyakati za dhiki.
12 “Je, mtu aweza kuvunja chuma,
chuma kinachotoka kaskazini, au avunje shaba?
13 “Utajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara,
bila gharama,
kwa sababu ya dhambi zako zote
katika nchi yako yote.
14 Nitakufanya uwe mtumwa wa adui zako
katika nchi usiyoijua,
kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa
utakaowaka juu yako daima.”
15 Wewe unafahamu, Ee Mwenyezi Mungu,
unikumbuke na unitunze mimi.
Lipiza kisasi juu ya watesi wangu.
Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali;
kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.
16 Maneno yako yalipokuja, niliyala;
yakawa shangwe yangu
na furaha ya moyo wangu,
kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,
Ee Bwana Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni.
17 Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe,
wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao;
niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako ulikuwa juu yangu,
na wewe ulikuwa umenijaza hasira.
18 Kwa nini maumivu yangu hayakomi,
na jeraha langu ni la kuhuzunisha,
wala haliponyeki?
Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu,
kama chemchemi iliyokauka?
19 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Ukitubu, nitakurejesha
ili uweze kunitumikia;
ukinena maneno yenye maana,
wala si ya upuzi,
utakuwa mnenaji wangu.
Watu hawa ndio watakaokugeukia,
wala si wewe utakayewageukia wao.
20 Nitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa,
ngome ya ukuta wa shaba;
watapigana nawe
lakini hawatakushinda,
kwa maana mimi niko pamoja nawe
kukuponya na kukuokoa,”
asema Mwenyezi Mungu.
21 “Nitakuokoa kutoka mikono ya waovu,
na kukukomboa kutoka makucha ya watu wakatili.”