47
Ujumbe kuhusu Wafilisti
1 Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza:
2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini,
yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana.
Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyo ndani yake,
miji na wanaoishi ndani yake.
Watu watapiga kelele;
wote wanaoishi katika nchi wataomboleza
3 kwa sauti ya kwato za farasi wanaoenda mbio,
kwa sauti ya magari ya vita ya adui,
na mngurumo wa magurudumu yake.
Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao,
mikono yao italegea.
4 Kwa maana siku imewadia
kuwaangamiza Wafilisti wote
na kuwakatilia mbali walionusurika wote
ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni.
Mwenyezi Mungu anakaribia kuwaangamiza Wafilisti,
mabaki toka pwani za Kaftori*yaani Krete.
5 Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza,
Ashkeloni atanyamazishwa.
Enyi mabaki kwenye tambarare,
mtajikatakata wenyewe hadi lini?
6 “Mnalia, ‘Aa, upanga wa Mwenyezi Mungu,
utaendelea hadi lini ndipo upumzike?
Rudi ndani ya ala yako;
acha na utulie.’
7 Lakini upanga utatuliaje
wakati Mwenyezi Mungu ameuamuru,
wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni
pamoja na pwani yake?”