48
Ujumbe kuhusu Moabu
Kuhusu Moabu:
 
Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo:
“Ole wake Nebo, kwa maana utaharibiwa.
Kiriathaimu utaaibishwa na kutekwa;
Misgabu itaaibishwa na kuvunjavunjwa.
Moabu haitasifiwa tena;
huko Heshboni watu watapanga jinsi ya kumwangusha:
‘Njooni na tuliangamize taifa lile.’
Wewe nawe, ee Madmena, utanyamazishwa;
upanga utakufuatia.
Sikiliza kilio kutoka Horonaimu,
kilio cha maangamizi makuu na uharibifu.
Moabu utavunjwa,
wadogo wake watapiga kelele.
Wanapanda kwenda njia ya kuelekea Luhithi,
wakilia kwa uchungu wanapotembea,
kwenye njia inayoshuka kwenda Horonaimu,
kilio cha uchungu kwa ajili ya uharibifu kinasikika.
Kimbieni! Okoeni maisha yenu,
kuweni kama kichaka jangwani.
Kwa kuwa mmetumainia matendo yenu na mali yenu,
ninyi pia mtachukuliwa mateka,
naye Kemoshi*mungu wa Wamoabu ataenda uhamishoni,
pamoja na makuhani wake na maafisa wake.
Mwangamizi atakuja dhidi ya kila mji,
wala hakuna mji utakaookoka.
Bonde litaangamizwa na uwanda utaharibiwa,
kwa sababu Mwenyezi Mungu amesema.
Wekeni chumvi kwa ajili ya Moabu,
kwa kuwa ataangamizwa;
miji yake itakuwa ukiwa,
hakutakuwa na mtu atakayeishi ndani yake.
 
10 “Alaaniwe yeye afanyaye kazi ya Mwenyezi Mungu kwa ulegevu!
Alaaniwe yeye auzuiaye upanga wake usimwage damu!
 
11 “Moabu amestarehe tangu ujana wake,
kama divai iliyoachwa kwenye machujo yake,
haikumiminwa kutoka chombo kimoja hadi kingine,
hajaenda uhamishoni.
Kwa hiyo ana ladha ile ile kama aliyokuwa nayo,
nayo harufu yake haijabadilika.
12 Lakini siku zinakuja,”
asema Mwenyezi Mungu,
“nitakapotuma watu wamiminao kutoka magudulia,
nao watamimina;
wataacha magudulia yake yakiwa matupu
na kuvunja mitungi yake.
13 Kisha Moabu atamwonea aibu Kemoshi,
kama vile nyumba ya Israeli walivyoona aibu
walipotegemea Betheli.
 
14 “Mwawezaje kusema, ‘Sisi ni mashujaa,
watu hodari katika vita’?
15 Moabu ataangamizwa na miji yake itavamiwa,
vijana wake wa kiume walio bora sana watachinjwa,”
asema Mfalme, ambaye jina lake
ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
16 “Kuanguka kwa Moabu kumekaribia,
janga kubwa litamjia kwa haraka.
17 Ombolezeni kwa ajili yake, ninyi nyote mnaomzunguka,
ninyi nyote mnaojua sifa zake,
semeni, ‘Tazama jinsi ilivyovunjika
fimbo ya kifalme yenye nguvu,
tazama jinsi ilivyovunjika
fimbo iliyotukuka!’
 
18 “Shuka kutoka fahari yako
uketi katika ardhi iliyokauka,
enyi wenyeji wa Binti Diboni,
kwa maana yeye aangamizaye Moabu
atakuja dhidi yako,
na kuangamiza miji yako yenye ngome.
19 Simama kando ya barabara na utazame,
wewe unayeishi Aroeri.
Muulize mwanaume anayekimbia
na mwanamke anayetoroka,
waulize, ‘Kumetokea nini?’
20 Moabu amefedheheshwa, kwa kuwa amevunjavunjwa.
Lieni kwa huzuni na kupiga kelele!
Tangazeni kando ya Mto Arnoni
kwamba Moabu ameangamizwa.
21 Hukumu imefika kwenye uwanda wa juu:
katika Holoni, Yahasa na Mefaathi,
22 katika Diboni, Nebo
na Beth-Diblathaimu,
23 katika Kiriathaimu, Beth-Gamuli
na Beth-Meoni,
24 katika Keriothi na Bosra;
kwa miji yote ya Moabu,
iliyo mbali na karibu.
25 Pembepembe inawakilisha nguvu ya Moabu imekatwa,
mkono wake umevunjwa,”
asema Mwenyezi Mungu.
 
26 “Mleweshe,
kwa kuwa amemdharau Mwenyezi Mungu.
Moabu atagaagaa katika matapishi yake,
awe kichekesho.
27 Je, Israeli hakuwa kitu chako cha kudhihakiwa?
Je, alikamatwa miongoni mwa wezi,
kiasi cha kutikisa kichwa chako kwa dharau
kila mara unapozungumza juu yake?
28 Ondokeni miji yenu, mkaishi katikati ya miamba,
enyi mnaoishi Moabu.
Kuweni kama njiwa ambaye hutengeneza kiota chake
kwenye mlango wa pango.
 
29 “Tumesikia kuhusu kiburi cha Moabu:
kutakabari kwake kwa kiburi na majivuno,
kiburi chake na ufidhuli wake,
na kujivuna kwa moyo wake.
30 Ninaujua ujeuri wake, lakini ni bure,”
asema Mwenyezi Mungu,
“nako kujisifu kwake hakumsaidii chochote.
31 Kwa hiyo namlilia Moabu,
kwa ajili ya Moabu yote ninalia,
ninaomboleza kwa ajili
ya watu wa Kir-Haresethi.
32 Ninalia machozi kwa ajili yenu, kama Yazeri aliavyo,
enyi mizabibu ya Sibma.
Matawi yako yameenea hadi baharini;
yamefika hadi bahari ya Yazeri.
Mwangamizi ameyaangukia
matunda yako yaliyoiva
na mizabibu yako iliyoiva.
33 Shangwe na furaha vimetoweka
kutoka bustani na mashamba ya Moabu.
Nimekomesha kutiririka kwa divai kutoka mashinikizo;
hakuna hata mmoja ayakanyagaye kwa kelele za shangwe.
Ingawa kuna kelele,
sio kelele za shangwe.
 
34 “Sauti ya kilio chao inapanda
kutoka Heshboni hadi Eleale na Yahazi,
kutoka Soari hadi Horonaimu na Eglath-Shelishiya,
kwa kuwa hata maji ya Nimrimu yamekauka.
35 Nitakomesha wote katika Moabu
watoao sadaka mahali pa juu pa kuabudia,
na kufukiza uvumba kwa miungu yao,”
asema Mwenyezi Mungu.
36 “Kwa hiyo moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama filimbi;
unaomboleza kama filimbi kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.
Utajiri waliojipatia umetoweka.
37 Kila kichwa kimenyolewa
na kila mwenye ndevu zimekatwa;
kila mkono umekatwa
na kila kiuno kimevalishwa gunia.
38 Juu ya mapaa yote katika Moabu
na katika viwanja
hakuna kitu isipokuwa maombolezo,
kwa kuwa nimemvunja Moabu
kama gudulia lisilotakiwa na mtu yeyote,”
asema Mwenyezi Mungu.
39 “Tazama jinsi alivyovunjikavunjika!
Jinsi wanavyolia kwa huzuni!
Tazama jinsi Moabu anavyogeuka kwa aibu!
Moabu amekuwa kitu cha kudhihakiwa,
kitu cha kutisha kwa wale wote
wanaomzunguka.”
40 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Tazama! Tai anashuka chini,
akitanda mabawa yake juu ya Moabu.
41 Miji itatekwa na ngome zake
zitatwaliwa.
Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Moabu
itakuwa kama moyo wa mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
42 Moabu ataangamizwa kama taifa
kwa sababu amemdharau Mwenyezi Mungu.
43 Hofu kuu, shimo na mtego vinawangojea,
enyi watu wa Moabu,”
asema Mwenyezi Mungu.
44 “Yeyote atakayeikimbia hiyo hofu kuu
ataanguka ndani ya shimo,
yeyote atakayepanda kutoka shimoni,
atanaswa katika mtego,
kwa sababu nitailetea Moabu
mwaka wa adhabu yake,”
asema Mwenyezi Mungu.
 
45 “Katika kivuli cha Heshboni,
wakimbizi wamesimama pasipo msaada,
kwa kuwa moto umezimika huko Heshboni,
Mwali wa moto kutoka katikati ya Sihoni;
unaunguza paji za nyuso za Wamoabu,
mafuvu ya wanaojivuna kwa kelele.
46 Ole wako, ee Moabu!
Watu wa Kemoshi wameangamizwa;
watoto wako wa kiume wamepelekwa uhamishoni,
na binti zako wamechukuliwa mateka.
 
47 “Lakini nitarudisha mateka wa Moabu,
katika siku zijazo,”
asema Mwenyezi Mungu.
Huu ndio mwisho wa hukumu ya Moabu.

*48:7 mungu wa Wamoabu

48:25 pembe inawakilisha nguvu