9
Isa amponya mtu aliyezaliwa kipofu
1 Isa alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. 2 Wanafunzi wake wakamuuliza, “Mwalimu, ni nani aliyetenda dhambi; ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”
3 Isa akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake. 4 Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi. 5 Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”
6 Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule kipofu machoni. 7 Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu” (Siloamu maana yake ni Kutumwa). Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona.
8 Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?” 9 Wengine wakasema, “Ndiye.”
Wengine wakasema, “Siye, bali anafanana naye.”
Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.”
10 Wakamuuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?”
11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Isa alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia, ‘Nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu,’ ndipo nikanawa nami nikapata kuona!”
12 Wale wakamuuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?”
Akawajibu, “Sijui.”
Mafarisayo wachunguza kuponywa kwa kipofu
13 Wakamleta yule mtu aliyekuwa kipofu hapo awali kwa Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.. 14 Basi siku hiyo Isa alitengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato. 15 Mafarisayo nao wakaanza kumuuliza yule mtu alivyopata kuona. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.”
16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.”
Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika.
17 Hivyo wakamwambia tena yule mtu aliyekuwa kipofu, “Wewe ndiwe uliyefumbuliwa macho. Wasemaje kuhusu mtu huyo?”
Yeye akawajibu, “Yeye ni nabii.”
18 Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu akapata kuona, hadi walipowaita wazazi wake. 19 Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?”
20 Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu. 21 Lakini hatujui jinsi anavyoweza kuona sasa, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Muulizeni; yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.” 22 Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi, kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu yeyote atakayemkiri Isa kuwa ndiye Al-Masihi†Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. atafukuzwa kutoka sinagogi. 23 Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni.”
24 Hivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.”
25 Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.”
26 Wakamuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?”
27 Akawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?”
28 Ndipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake! Sisi ni wanafunzi wa Musa. 29 Tunajua kwamba Mungu alisema na Musa, lakini mtu huyu hatujui anakotoka.”
30 Yule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu! 31 Tunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii. 32 Tangu zamani hatujasikia kwamba mtu amemponya yeyote aliyezaliwa kipofu. 33 Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lolote.”
34 Wakamjibu, “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, nawe unajaribu kutufundisha?” Wakamfukuza atoke nje.
Upofu wa kiroho
35 Isa aliposikia kuwa wamemfukuza atoke nje yule mtu aliyemfumbua macho, alimkuta, akamuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”
36 Yule mtu akamjibu, “Yeye ni nani, Bwana‡Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida.? Niambie ili nipate kumwamini.”
37 Isa akamjibu, “Umekwisha kumwona; naye anayezungumza nawe, ndiye.”
38 Yule mtu akasema, “Bwana, naamini.” Naye akamwabudu.
39 Isa akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona wawe vipofu.”
40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?”
41 Isa akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.
*9:13 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.
†9:22 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.
‡9:36 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida.