10
Mchungaji mwema
1 “Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang’anyi. 2 Yeye anayeingia kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo. 3 Mlinzi humfungulia lango, na kondoo huisikia sauti yake. Yeye huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi. 4 Baada ya kuwatoa wote nje, yeye hutangulia mbele yao na kondoo humfuata, kwa kuwa wanaijua sauti yake. 5 Lakini kondoo hawatamfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.” 6 Isa alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia.
7 Kwa hiyo Isa akasema nao tena, akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. 8 Wote walionitangulia ni wezi na wanyang’anyi, nao kondoo hawakuwasikia. 9 Mimi ndimi lango. Yeyote anayeingia zizini kupitia kwangu ataokoka. Ataingia na kutoka, naye atapata malisho. 10 Mwizi huja ili aibe, aue na aangamize. Mimi nimekuja ili wapate uzima, kisha wawe nao tele.
11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Anapomwona mbwa-mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa-mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. 13 Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.
14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu, nao kondoo wangu wananijua. 15 Kama vile Baba*Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, ndivyo nami ninautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili. Inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu; hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. 17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. 18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu, na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”
19 Waliposikia maneno haya, Wayahudi wakagawanyika. 20 Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.”
21 Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”
Isa akataliwa na Wayahudi
22 Ikafika Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu†yaani Hanukkah kwa Kiebrania huko Yerusalemu. Ilikuwa majira ya baridi. 23 Naye Isa alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika Ukumbi wa Sulemani. 24 Wayahudi wakamkusanyikia, wakamuuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka hadi lini? Kama wewe ndiwe Al-Masihi‡Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., tuambie waziwazi.”
25 Isa akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia. 26 Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu. 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata. 28 Nami ninawapa uzima wa milele; hawataangamia kamwe, wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu. 29 Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote, na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake. 30 Mimi na Baba yangu tu umoja.”
31 Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo, 32 lakini Isa akawaambia, “Nimewaonesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni kwa ipi kati ya hiyo miujiza mnataka kunipiga mawe?”
33 Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Ingawa wewe ni mwanadamu, unajifanya kuwa Mungu.”
34 Isa akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Torati yenu kwamba, ‘Nimesema kuwa ninyi ni “miungu” ’? 35 Kama aliwaita ‘miungu’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka, 36 je, mwawezaje kusema kwamba yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru, kwa sababu nilisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu§Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.’? 37 Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini. 38 Lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ni ndani yake.” 39 Ndipo wakajaribu kumkamata kwa mara nyingine, lakini akaponyoka kutoka mikononi mwao.
40 Isa akaenda tena ng’ambo ya Yordani hadi mahali Yahya alikuwa akibatiza hapo awali, naye akakaa huko. 41 Watu wengi wakamjia, nao wakawa wakisema, “Yahya hakufanya muujiza wowote, lakini kila jambo alilosema kumhusu huyu mtu ni kweli.” 42 Nao watu wengi wakamwamini Isa huko.